ICRC: Vituo vya afya vimeelemewa mno huko Gaza
18 Julai 2024Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imesema kuwa hospitali yake ndogo katika mji wa Rafah imekuwa ikipokea idadi kubwa ya wagonjwa wanaohitaji kulazwa hospitalini kutokana na majeraha yanayosababishwa na mashambulizi.
Shirika hilo la kimataifa limesema kuwa hospitali nyingi katika eneo hilo zimeelemewa, jambo ambalo litapelekea hivi karibuni madaktari kulazimika kufanya "maamuzi magumu" ya kuchagua ni nani anayepaswa au la kutibiwa.
Soma pia: Israel yaendeleza mashambulizi Gaza licha ya ukosoaji wa Marekani
Wiki iliyopita, watu 850 wanaohitaji huduma waliwasili katika hospitali hiyo inayomilikiwa na shirika la Msalaba Mwekundu, huku karibu nusu ya watu hao wakiwa ni wanawake na theluthi moja wakiwa ni watoto.
Taarifa ya shirika hilo imebainisha kuwa wagonjwa wengi wamehamishwa kutoka kwenye makazi yao na wamekuwa wakiishi katika mazingira duni yenye msongamano wa watu na yanayokabiliwa na uhaba wa chakula na maji safi, jambo linalowaweka hatarini zaidi kupata magonjwa.
Kiongozi wa Israel ashinikiza kuendeleza mashambulizi
Waziri wa Usalama wa Israel na mwenye siasa kali za mrengo wa kulia Itamar Ben Gvir, ameutembelea leo msikiti wa Al Aqsa huko Jerusalem ambao umekuwa kiini cha mvutano kati ya Israel na Palestina na kusema:
"Nimekuja hapa, mahali muhimu kwa taifa la Israel, kwa watu wa Israel, mnatakiwa kuwaombea mateka warudi nyumbani lakini si kwa makubaliano ya kizembe, bila kujisalimisha. Ninaomba na pia kufanya kazi kwa bidii ili Waziri Mkuu Netanyahu awe na ujasiri wa kutoachia msimamo wake na kuelekea kwenye ushindi kwa kuongeza shinikizo la kijeshi, na kuzima ari ya Hamas kushinda."
Kauli ya Ben Gvir imetafsiriwa kuwa huenda inatishia kuvuruga mchakato unaoendelea wa mazungumzo ya usitishwaji mapigano, hasa wakati huu mashambulizi ya Israel yakiendelea kuripotiwa sehemu mbalimbali huko Gaza.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema hivi leo kwamba umwagaji damu huko Gaza ni lazima usitishwe sasa, akiongeza kuwa raia wengi mno katika eneo la Palestina wamepoteza maisha yao kutokana na jibu la Israel kwa ugaidi wa kikatili wa Hamas. Von der Leyen alikamilisha kwa kusema, watu wa Gaza hawawezi kuvumilia zaidi na ubinadamu hauwezi tena kustahimili.
(Vyanzo: Mashirika)