1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiSudan

Wakazi wa Khartoum wahatarisha maisha yao kutafuta maji safi

30 Mei 2023

Mapigano nchini Sudan yamewaacha maelfu ya wakaazi wa jiji la Khartoum bila maji safi huku wengine wakilazimika kuhatarisha hadi maisha yao kwa kutafuta bidhaa hiyo muhimu kunaposhuhudiwa utulivu wa muda mfupi.

https://p.dw.com/p/4RxF0
Sudan, Khartoum | Menschen versammeln sich zum Wasser holen
Picha: Marwan Ali/AP/picture alliance

Baada ya takriban wiki sita za makabiliano kati ya vikosi vya majenerali hasimu na hali ya joto kali inayoweza kufikia hadi nyuzi joto 40, wakazi wengi wa vitongoji vya kaskazini mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum wana uhitaji mkubwa wa maji safi ya kunywa.

Mnamo Aprili 15, wakati mapigano yalipozuka kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), kituo kinachosambaza maji safi katika wilaya kadhaa za Khartoum Kaskazini kiliharibiwa.   

Tangu wakati huo, wakazi wa eneo hilo wapatao 300,000 hawajaona hata tone la maji likitoka kwenye mabomba yao. Wengine wamelazimika kuanza kutumia visima na kuteka maji kutoka kwenye Mto Nile.

Mkazi wa Khartoum Adel Mohammed ameliambia shirika la habari la AFP kwamba mwanzoni mwa vita, walichukua maji kutoka kwenye visima katika eneo la viwanda, lakini baada ya wiki moja tu, wanamgambo walichukua udhibiti wa maeneo hayo.   

Wakati mapambano yakipamba moto maeneo hayo na mapigano yakifanyika katika majengo ya makazi na hospitali, Mohammed hulazimika kusubiri siku kadhaa kabla ya kuweza kujitosa na kwenda kusaka maji.

   Soma pia: Umoja wa Mataifa watoa tahadhari ya njaa Haiti, Sahel na sudan  

Yeye na majirani zake husubiri mapigano yapungue kwa muda mfupi ili waweze kuchukua vifaa mbalimbali kama beseni na mitungi hadi kwenye kingo za Mto Nile, unaopita katika vitongoji vya mji wa Khartoum. Kwa pamoja, hupakia madumu hayo ya maji kwenye gari na baadaye kusambaza lita chache za maji kwa kila familia zilizo jirani. Lakini wakazi wengi wameondoka eneo hilo.

     

Rashed Hussein, ambaye alikimbia na familia yake kwenda Madani, takriban kilomita 200 kusini mwa Khartoum, amesema kilichopelekea yeye kuchukua uamuzi wa kuondoka na kuiacha nyumba yake ni ukosefu wa maji safi na wala sio milipuko ya mabomu na mapigano. Hussein, akiwa ni mmoja wa Wasudan zaidi ya milioni moja waliokimbia makazi yao kufuatia vita hivi, amesema hawezi kuvumilia kuwaona watoto wake wakiishi bila maji safi ya kunywa au kuoga.

 

Uhaba wa maji ni tatizo la muda mrefu Sudan

Sudan | Kämpfe in Khartum
Wakazi wa Khartoum wakijaribu kutafuta maji safi (25.05.2023)Picha: AFP/Getty Images

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, hata kabla ya vita, Wasudan wapatao milioni 17.3 walikuwa na uhaba wa maji safi ya kunywa. Shirika hilo limeendelea kubaini kuwa magonjwa yatokanayo na uhaba wa maji na hali duni ya usafi ndio sababu kuu za vifo vya watoto walio na umri chini ya miaka mitano.      

Salah Mohammed, mkaazi mwingine wa  Kaskazini mwa Khartoum,  alisalia eneo hilo licha ya mapigano na alikuwa akipata maji kwa kutumia kisima katika hospitali iliyo karibu, ambayo ilitumia pia maji hayo kwa wagonjwa. Lakini wiki moja baadaye, wanamgambo wa RSF walichukua udhibiti wa hospitali hiyo, na hakuweza tena kupata maji kutoka kituo hicho cha afya.

Rashida al-Tijani anaishi karibu na hospitali nyingine, ambako pia anaweza kupata maji. Husubiri makabiliano ya risasi yapungue ili kwenda hospitalini haraka iwezekanavyo na kuchukua maji mengi awezavyo kwa ajili ya familia yake. al-Tijani amesema hajaweza kufua nguo hata moja tangu kuanza kwa vita hivyo.

Maisha ya kila siku na hata uchumi wa Sudan vimesimama tangu mzozo huo ulipozuka, na hivyo kutatiza miundombinu na huduma za umma ambavyo tayari ni duni nchini humo. Watumishi wa umma wako likizo kwa muda usiojulikana huku wapiganaji wakichukua udhibiti wa hospitali, viwanda na majengo ya umma.

    Soma pia: Mapigano yaendelea Khartoum licha ya kuwepo kwa mkataba wa usitishaji mapigano  

Mitandao isiyo rasmi ya vikundi vya mtaa, vinavyojulikana kama kamati za upinzani, wamehamasishwa kuanzisha hospitali na vituo vya usambazaji wa chakula na maji safi. Awali kamati hizi zilijipanga kabla ya vita ili kupinga udhibiti wa jeshi katika mamlaka za kisiasa.

      

Mjumbe mmoja wa kamati hiyo, ambaye hakupenda kutajwa jina kwa kuhofia madhara kutoka kwa jeshi au vikosi vya RSF, amesema tangu kuanza kwa vita, wamekuwa wakiwapa wakazi maji, na kusema kuwa katika safari moja ya kutafuta maji, rafiki yao Yassine aliuliwa kwa risasi.

      

Mjumbe wa kamati hiyo amesema maji nchini Sudan yamekuwa tatizo kubwa hata mtu anapofariki. Anasema walilazimika kumzika rafiki yao huyo bila ya kuuosha mwili wake.

(Afpe)