Israel na Hezbollah washambuliana maeneo muhimu
24 Oktoba 2024Katika taarifa yake, jeshi la Israel limesema limefanya mashambulizi ya anga usiku kucha katika maeneo linayodai ni muhimu kwa wanamgambo wa Hezbollah, vikiwemo vituo kadhaa vya kuhifadhi na kutenegeza silaha katika eneo la Dahiyeh.
Vyombo vya habari nchini Lebanon vimeripoti kwamba takribani majengo sita yalishambuliwa na kuharibiwa vibaya kwenye mashambulizi hayo ya anga ya Israel.
Kwa mara nyingine tena Israel imerejelea madai yake kwamba majengo ya raia yaliyoshambuliwa yalitumiwa na wanamgambo wa Hizbullah katika kuhifadhi silaha, tuhuma zile zile ambazo imekuwa ikizitumia kwenye vita vyake katika Ukanda wa Gaza.
Soma pia:Israel yasema ilimuuwa afisa wa Hezbollah aliyetarajiwa kuwa kiongozi wa kundi hilo
Kwa upande wake, Hizbullah imesema imefanya mashambulizi ya kujibu mapigo ya adui. Katika mashambulizi hayo, kundi hilo linaloungwa mkono na Iran limevurumisha mkururo wa maroketi na kulenga kambi ya kijeshi kaskazini mwa mji wa Haifa ikiwa ni mara ya pili ndani ya masaa 24 kulengwa kwa kambi hiyo.
Makombora ya Hizbullah yalishambulia pia kambi za kutengeneza silaha na kusababisha hali katika eneo hilo kuwa tete zaidi kiusalama kwa raia.
Israel yawauwa wanajeshi wa Lebanon wakiokoa raia
Kufuatia kuongezeka kwa mashambulizi ya Israel maeneo ya kusini mwa mji mkuu, Beirut, jeshi la Lebanon limesema wanajeshi wake watatu wameuwawa wakati walipokuwa kwenye operesheni ya kuwaokoa raia na majeruhi wengine.
Aidha shirika la habari la Lebanon, NNA, limeripoti kwamba watu kadhaa wameuwawa huku wahudumu wa afya wakijeruhiwa kufuatia mashambulizi hayo.
Kulingana na mamlaka nchini Lebanon zaidi ya watu 2,500 wameuwawa kufuatia mashambulizi ya Israel huku zaidi ya watu milioni moja wakiyakimbia makaazi yao tangu mwezi Septemba mwaka huu.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alimwambia mwenzake wa Israel jana Jumatano kwamba Washington ina wasiwasi kuhusu mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Lebanon huku akiitaka Israel kuchukua hatua kuhakikisha usalama wa jeshi la Lebanon na ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon.
Soma pia:Hezbollah yadai kuhusika na shambulizi la droni kwenye nyumba ya Netanyahu
Katika juhudi za kimataifa kuhakikisha misaada ya kiutu kwa Walebanon, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema nchi yake itachangia kiasi cha yuro milioni 100 kuelekea lengo la kufikisha kiasi cha yuro milioni 500 ili kuwasaidia watu waliokimbia mapigano Lebanon.
Macron amesema hayo katika mkutano wa kimataifa wa kuhusu Lebanon unaolenga kuchangisha fedha kwa ajili ya misaada na kusisitiza kwamba lazima vita kati ya kundi la Hezbollah na Israel vikomeshwe mara moja.
"Ufumbuzi lazima upatikane haraka kwa sababu ni lazima kwa gharama yoyote ile tuzuie kuhama kwa watu kutoka kusini, Beirut na maeneo mengine ya Lebanon."
Katika mkutano huo Ujerumani kupitia waziri wake wa Mambo ya Nje Annalena Baerbock imeahidi kuchangia kiasi cha yuro milioni 96 kwa ajili ya msaada wa kiutu Lebanon.
Blinken atua Qatar kusaka suluhu Gaza
Ama katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amewasili Qatar kwa ajili ya mazungumzo na mpatanishi mkuu wa vita vya Gaza katika wakati ambapo akitafuta usitishaji wa mapigano, baada ya Israel kumuua kiongozi wa Hamas, Yahya Sinwar.
Soma pia:Blinken asema "sasa ni wakati" wa kuvimaliza vita vya Gaza
Blinken anakutana na wapatanishi hao baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem, kisha anakutana na viongozi wa Qatar akiwemo Mfalme Shekhe Tamim bin Hamad Al-Thani na Waziri Mkuu Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al-Thani kwa ajili ya kutathmini msimamo wa Hamas kwenye makubaliano hayo.