1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Janga la COVID-19 kuzidisha madhila ya watoto wakimbizi

3 Septemba 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR limesema nusu ya watoto wote wakimbizi duniani, walikuwa tayari hawaendi shuleni kabla ya janga la virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3hx9X
BG Pink Lady Food Photographer of the Year 2020 | K M Asad
Picha: K M Asad

Shirika hilo limeonya kuwa janga hilo huenda likasababisha mgogoro mkubwa zaidi na kuwapokonya mamilioni ya watoto nafasi ya kujitengezea maisha yao ya baadae. 

Ripoti mpya ya shirika hilo la UNHCR imeonya kuwa watoto wengi wa wakimbizi, hasa wale wa kike waliohudhuria shule kabla ya janga la virusi vya corona kuitikisa dunia, huenda wasirejee tena shuleni. Filippo Grandi Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo akitoa wito wa kuunga mkono mpango wa haki ya elimu kwa wakimbizi amesema Baada ya wakimbizi hao kupitia mambo mengi haitowezekana kuwapokonya maisha yao ya baadae kwa kuwanyima fursa ya kwenda shule.

Ripoti hiyo inayotumia data kutoka nchi 12 zinazotoa hifadhi kwa zaidi ya nusu ya idadi ya wakimbizi duniani, imegundua kuwa watoto wakimbizi milioni 1.8 au asilimia 48 wanaopaswa kwenda shule hawapati huduma hiyo muhimu, na ushiriki wa watoto hao katika shule za sekondari au masomo ya juu zaidi ni mdogo mno. Asilimia 77 ya watoto wakimbizi walisajiliwa kwenda shule lakini ni asilimia 31 moja pekee wanaokwenda shule za sekondari na asilimia tatu tuu ndio wanahudhuria masomo ya juu, hii ikiwa ni kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Uganda Flüchtlingslager Palorinya Südsudan
Wakimbizi wa Sudan Kusini miongoni mwao watoto wakiwasili Uganda Picha: DW/L. Emmanuel

UNHCR imesema ubadilishaji wa mbinu umeifanya kuwa ngumu zaidi kulinganisha data za mwaka huu na mwaka uliopita lakini makadirio madogo yanaonesha uboreshaji au maendeleo ya masomo kwa watoto hao. Kulingana na ripoti ya mwaka 2019 asilimia 1 tu ya watoto wakimbizi duniani walihudhuria masomo ya juu. Lakini kwa sasa janga la virusi vya corona linatishia hali kuwa mbaya zaidi.

Ripoti hiyo imeendelea kusema kwamba wakati watoto katika kila nchi wakikumbwa na madhara ya ugonjwa wa COVID 19 kutokana na masharti yaliowekwa kujaribu kudhibiti kuenea zaidi kwa virusi vya corona, watoto wa wakimbizi wameathirika zaidi na kukosa nafasi hiyo ya kujiendeleza kimasomo. Soma Mtoto mmoja kati ya wanne duniani wanaishi katika mazingira ya vita

Watoto hao wanasemekana kupitia changamoto kubwa zaidi kuliko wengine kurejea masomoni, huku familia nyingi zikikosa kumudu ada ya shule ya watoto wao, sare za shule pamoja na vitabu kufuatia kupungua kwa vipato vya wazazi. Watoto hao pia hawana urahisi ya kufikia teknolojia inayohitajika kuendelea na masomo na huenda wakalazimika kufanya kazi ili kuendelea kusaidia familia zao kujimudu kimaisha.

Ikitumia data kutoka UNHCR mfuko wa Malala unaojishughulisha na suala la kuondoa vizingiti vya kwenda shule kwa mtoto wa kike, umekadiria kuwa nusu ya watoto wa kike ambao walikuwa wanakwenda shule kabla ya janga la virusi vya corona sasa huenda wasifike katika majengo hayo kabisa wakati shule zitakapofunguliwa mwezi huu. Na katika mataifa ambayo chini ya asilimia 10 ya watoto wa kike wakimbizi walisajiliwa kwenda shule ya sekondari, wote wapo katika hatari ya kuacha kabisa masomo yao. UNHCR imesema hatua hiyo inatisha na huenda ikaathiri kizazi kijacho.