Korea Kaskazini yafyatua makombora
19 Oktoba 2021Huku haya yakijiri wakuu wa ujasusi wa Marekani, Japan na Korea Kusini wakutana kujadili mkwamo kwenye mazungumzo ya mpango wa silaha za nyuklia wa Korea Kaskazini.
Hatua hii ni ya hivi karibuni kwa Korea Kaskazini kujaribu silaha zake na kuendeleza ajenda ya kuimarisha uwezo wake wa kijeshi, wakati ikikabiliwa na vikwazo vya kimataifa iliyovyowekewa kutokana na programu yake ya silaha za nyuklia na makombora. Soma zaidi Korea Kaskazini yajaribu makombora mapya ya masafa marefu
Korea kusini iko tayari kushirkiana na Marekani
Katika taarifa yake, Korea Kusini imesema inafuatilia kwa karibu hali hiyo na kuimarisha utayari wake kwa kushirikiana na Marekani, endapo kutakuwa na urushaji wa makombora mengine.
Kulingana na taarifa ya pamoja kutoka kwa wakuu wa kijeshi, kombora moja lilirushwa saa nne na dakika kumi na saba asubuhi kutoka maeneo ya Sinpo, sehemu ambayo Korea Kaskazini huweka manowari na vile vile vifaa vya kufyatulia makombora ya masafa marefu.
Gazeti la Korea Kusini, Joongang Ilbo, limemnukuu afisa mmoja wa jeshi bila kumtaja jina akisema kwamba serikali inakisia tu kwamba urushaji wa kombora hilo ulikuwa jaribio, lakini hakutoa maelezo zaidi.
Baraza la usalama la Korea Kusini limefanya mkutano wa dharura na kuelezea "masikitiko makubwa" juu ya jaribio hilo na badala yake likaitaka Korea Kaskazini kurudi katika mazungumzo. Soma Korea Kaskazini kushinikizwa kuingia mazungumzo ya nyuklia
Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida amesema mabaki ya makombora mawili ya masafa marefu yamegunduliwa, huku akikitaja kitendo cha Korea Kaskazini kurusha makombora hayo kuwa "cha kusikitisha".
Idadi ya makombora yaliyofyatuliwa
Hata hivyo, hakujakuwa na maelezo ya mara moja kutoka kwa wakuu wa jeshi wa Korea Kusini juu ya idadi kamili ya makombora yaliyogundulika kufyatuliwa.
Wizara ya Muungano ya Korea Kusini, ambayo inashughulikia uhusiano wake na Korea Kaskazini, imesema mawasiliano ya kawaida ya kila siku na Kaskazini yamefanywa leo hii na hakukuwa na maoni juu ya urushaji wa makombora.
Jeshi la Marekani kwa upande wake linaona urushaji huo wa makombora ya Korea Kaskazini unaondoa utulivu lakini sio tishio la haraka kwa Marekani au washirika wake. Soma Kim ailaumu Marekani kwa kuzorotesha usalama rasi ya Korea
Taarifa kutoka kamandi ya jeshi la Marekani katika Bahari ya Pasifiki imesema kwamba Marekani imelaani vitendo hivi na imetoa wito kwa Korea Kaskazini kujiepusha na vitendo vyovyote vya kuondoa utulivu.
Vyanzo:Reuters/AFPE