Korea Kaskazini yasema inaiunga mkono Urusi hadi mwisho
1 Novemba 2024Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini Choe Son Hui yuko ziarani nchini Urusi ambako ameahidi kuwa nchi yake itasimama na Urusi hadi pale nchi hiyo itakaposhinda vita vyake dhidi ya Ukraine. Wakati huo huo Ukraine imeripoti kuwa Urusi imeishambulia miji yake kwa zaidi ya droni 2000 katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini alikuwa akizungumza na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov mjini Moscow na kumuahidi kwamba nchi yake inasimama bega kwa bega na Urusi katika mapambano yake ya vita na Ukraine.
Soma zaidi.Korea Kaskazini yasema itasimama na Urusi hadi ipate ushindi Ukraine
Choe pia alitumia jukwaa hilo kuishutumu Marekani na washirika wengine wa Magharibi wa Ukraine kwa kuvifanya vita hivyo kuwa vya muda mrefu dhidi ya Urusi kwa kuipatia Ukraine silaha.
Alipokuwa akielezea msimamo wa Korea Kaskazini kwa Urusi, Choe amesema "Mahusiano yetu ya jadi ya kihistoria ambayo yamepita njia ngumu, leo, shukrani kwa uongozi makini na wenye nguvu wa Rais wetu wa Korea Kim Jong Un, na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, yamefikia kiwango kipya cha ushirikiano wa kijeshi usioweza kushindwa, na vile vile uhusiano wa kimkakati wenye mtazamo wa miaka 100''.
Kwa upande wake, Mwenyeji wake, Sergei Lavrov, Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi yeye ameusifu uimara wa mahusiano baina ya nchi hizo mbili.
"Uhusiano wa nchi mbili kati ya nchi zetu umefikia kiwango cha juu sana katika miaka michache iliyopita kutokana na umakini maalum uliotolewa kwa uhusiano huu na Rais Putin na Kim Jong Un."amesema Lavrov.
Marekani yasema wanajeshi wa Korea Kakazini wako Kursk
Katikati mwa wiki hii Ikulu ya Marekani ilisema kuwa wanajeshi 8,000 wa Korea Kaskazini walikuwa wametumwa katika eneo la Kursk la Urusi kwenye mpaka na Ukraine, eneo ambalo kwa sasa linadhibitiwa na wanajeshi wa Ukraine.
Marekani inaamini kuwa majeshi yaKorea Kaskaziniyatatumwa hivi karibuni kupambana nchini Ukraine.
Rais Putin wa Urusi mpaka sasa hajakanusha taarifa hizo huku akisema kuwa hata Ukraine pia imekuwa ikisaidiwa na wanajeshi kutoka nchi wanachama wa NATO.
Soma zaidi. Korea Kaskazini yarusha kombora la ICBM wakati Marekani, Seoul zikiisokoa kutuma jeshi Urusi
Katika hatua nyingine, Jeshi la Ukraine limeripoti leo kuwa Urusi ilifanya zaidi ya mashambulizi 2,000 ya droni kote nchini humo katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa droni 1,185 kati ya 2,023 zilidunguliwa. Kwa sasa Ukraine inajiandaa kwa msimu mwingine wa kukatika kwa umeme huku kukiwa na tishio la mashambulizi mapya ya Urusi kwenye mfumo wa nishati wa nchi ambayo tayari ilikuwa imedhoofishwa na mfululizo wa mashambulizi ya mapema mwaka huu.