Maelfu waandamana kutaka Ufaransa iondoe vikosi vyake Niger
3 Septemba 2023Waandamanaji hao walikusanyika karibu na kambi ya wanajeshi wa Ufaransa baada ya mashirika kadhaa ya kiraia kutoa wito wa maandamano dhidi ya wanajeshi wa Ufaransa nchini humo. Walionekana wakiwa wameshika mabango yanayosomeka " Wanajeshi wa Ufaransa, ondokeni nchini mwetu"
Maandamano hayo yalizidi kuwa makubwa kutokana na waandamanaji wapya kuwasili- mchana na umati mkubwa uliokuwa katika makutano ya barabara karibu na kambi ya wanajeshi wa Ufaransa nje kidogo ya mji mkuu Niamey.
Soma zaidi: Niger yajiandaa na maandamano makubwa ya kuipinga Ufaransa
Utawala wa kijeshi wa Niger, Ijumaa uliituhumu Ufaransa kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi kwa kumuunga mkono Rais aliyepinduliwa, Mohamed Bazoum. Rais huyo mshirika wa Ufaransa ambaye kuchaguliwa kwake kulileta matumaini ya utulivu katika taifa hilo alikamatwa na wajumbe wa kitengo chake cha ulinzi Julai 26.
Uhusiano na Ufaransa wazidi kuzorota
Uhusiano wa Niamey na Ufaransa ambayo ni mkoloni wake wa zamani ulitetereka baada ya Paris kuchagua kuwa upande wa Bazoum.
Agosti 3, utawala huo wa kijeshi ulitangaza kuvunja makubaliano ya kijeshi na Ufaransa ambayo ina wanajeshi wasiopungua 1,500 Niger, hatua ambayo Ufaransa imeipuuzia kwa misingi ya kukosa uhalali.
Utawala wa kijeshi wa Niger, ulitangaza pia kumfukuza mara moja balozi wa Ufaransa nchini humo, Sylvain Itte na umemvua kinga ya kidiplomasia. Umesema kuwa, uwepo wa balozi huyo ni kitisho kwa utaratibu wa umma. Hata hivyo rais Emmanuel Macron siku ya Jumatatu alimpongeza Itte kwa kazi yake Niger na kuongeza kuwa angeendelea kubaki nchini humo licha ya kupewa saa 48 kuondoka nchini humo.
Kifungu cha 22 cha Azimio la Uhusiano wa Kimataifa la Vienna cha mwaka 1961 kinasema kuwa, majengo ya ubalozi hayaguswi na kwamba maafisa wa taifa mwenyeji hawana ruhusa ya kuingia kwenye maeneo hayo isipokuwa kwa idhini ya mkuu wa misheni.