1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabadiliko ya tabianchi, chanzo cha mafuriko DRC

14 Desemba 2022

Rais Felix Thisekedi wa Jamhuri wa Kidemokrasia ya Kongo amehusisha athari za mabadiliko ya tabinachi na mafuriko makubwa yaliyolikumba taifa lake na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 100 katika mji mkuu, Kishansa.

https://p.dw.com/p/4Ktks
USA UN Generalversammlung in NY l Rede des kongolesischen Präsidenten Tshisekedi
Picha: Angela Weiss/AFP

Barabara kuu katika mji huo mkuu zilifungwa kwa masaa kadhaa baada ya kufunikwa na maji na kusababisha usumbufu mkubwa. 

Kinshasa inakaliwa na wakazi milioni 15. Idadi ya watu waliofariki kutokana na mafuriko hayo ilikadiriwa kufikia 120 hadi usiku wa jana. Serikali imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuanzia hii leo, hii ikiwa ni kulingana na ofisi ya waziri mkuu Jean-Michel Sama Lukonde.

Mkuu wa jeshi la polisi Sylvano Kasongo ameliambia shirika la habari la AFP wengi wa waliofariki walikuwa wakiishi katika maeneo ya milimani ambako kulikumbwa na maporomoko ya udongo. Mwandishi wa habari wa AFP ameshuhudia miili ya watu tisa wa familia moja ikiwa ni pamoja na watoto waliofariki baada ya kuangukiwa na nyumba iliyoshindwa kuhimili kishindo cha maji katika mtaa wa Binza Delvaux.

USA | US-Afrika Gipfel | Antony blinken und Felix Tshisekedi
Rais Felix Tshisekedi ni miongoni mwa wakuu wa Afrika walioko Marekani kwa ajili ya mkutano wa wakuu wa Mataifa hayo na MarekaniPicha: Evelyn Hockstein/Pool via AP/picture alliance

Akiwa Washington, rais Tshisekedi amemwambia waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken katika mkutano kati ya Marekani na viongozi wa Afrika, kwamba DRC inakabiliwa na shinikizo kubwa, lakini ni bahati mbaya kwamba hakuna anayesikia wala kuisaidia.

"Kwa kuwa tumekusanyika hapa kuzungumzia vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, mkiniruhusu ningependa kuwataarifu kwa masikitiko makubwa kuhusu janga lililoikumba nchi yangu, ya kwamba Congo imekumbwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa zilizochochewa na mzozo wa mabadiliko ya tabianchi na kusababisha vifo vya mamia ya watupamoja na uharobifu mkubwa wa mali ambao ungeweza kuepukika kama makubaliano ya kuzuia uchafuzi yaliyofikiwa miaka ya nyuma yangetekelezwa," amesema Tshisekedi.

Soma Zaidi:Maoni: Mazungumzo ya tabianchi, Afrika iko peke yake 

Kinshasa bado inakabiliwa na changamoto ya miundombinu finyu na idadi kubwa ya watu.

Tshiswkedi amesema ni lazima mataifa yanayochafua mazingira kutoa msaada, kwa kuwa hayo ndio chanzo cha uharibifu na athari kwa mataifa masikini yanayoshindwa kujilinda dhidi ya athari za mabadiliko hayo.

Blinken ametoa salamu za pole kufuatia vifo hivyo akisema mafuriko yalikuwa uthibitisho wa kina wa changamoto zinazoyakabili mataifa kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambazo kwa hakika zinahitaji nguvu ya pamoja ili kuzitatua.

DRK Kongo | Erdrutsch Starkregen Unwetter
Hali ni tetet katika jiji la Kinshasa baada ya mafuriko yaliyochochewa na mabadiliko ya tabianchiPicha: REUTERS

Kinshasa inakabiliwa na changamoto ya idadi kubwa ya watu wanaoingia kutoka maeneo mbalimbali, na makazi mengi ni ya mabanda yaliyojengwa katika maeneo ya miteremko ambayo yako hatarini kunapotokea mafuriko. Pamoja na hayo, jiji hilo lina changamoto kubwa ya mifereji ya kuondoa maji na mifumo ya maji taka.

Mwezi Novemba mwaka 2019, karibu watu 40 walikufa katika jiji hilo la Kinshasa kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo. Eneo la Mont-Ngafula liliathiriwa zaidi, ingawa wakazi wa eneo hilo wanasema hawajawahi kushuhudia mafuriko na athari kubwa kama zilizotokea hivi sasa. Mmoja ya wakazi anayeitwa Freddy anasema kila kitu kwenye nyumba yake kilifunikwa na maji, kuanzia chakula na kila kitu na hakuweza kuokoa chochote.

Kama wa kale walivyosema, kufa kufaana.. pembezoni mwa Freddy alikuwa mkazi mwingine aliyefanya kazi ya kuwabeba watu ambao hawakutaka kuchafuka kwa maji na tope zito lililosabaishwa na mvua hizo, ambao walilazimika kumlipa senti 24 za Kimarekani sawa na Faranga 500 ili kuvuka.

Soma Zaidi: Wajumbe wa COP27 waidhinisha mfuko wa kuzisaidia nchi maskini