Mabomu ya Gaddafi yaitikisa Misrata
18 Aprili 2011Mji wa Misrata umejikuta leo hii (18.04.2011) ukishambuliwa kwa kila namna na vikosi vya Gaddafi. Watunguaji waliojitega kwenye majengo marefu, mabomu ya mchawanyiko na mizinga imezua tafrani katika mji.
Kwa mujibu wa mashirika ya haki za binaadamu, mabomu ya mchawanyiko yamekuwa yakitumika na ni sababu ya vifo vingi kwa wakati mmoja.
Mkuu wa hospitali ya Misrata, Dokta Khaled Abu Falgha, amewaambia waandishi wa habari kwamba watu 17 waliuawa hapo jana tu. Abu Falgha amesema kuwa, ndani ya wiki hizi sita za vita, tayari watu 1,000 wameshafariki katika mji huo uliozingirwa na wengine 3,000 wamejeruhiwa. Asilimia 80 ya wahanga ni raia wa kawaida.
Serikali yakanusha
Hata hivyo, msemaji wa serikali ya Gaddafi, Moosa Ibrahim, amekanusha kuwa vikosi vya serikali vinaushambulia mji wa Misrata na kwamba vinatumia mabomu ya mchawanyiko ambayo yamepigwa marufuku katika nchi kadhaa duniani.
"Tunafadhaishwa kuwa mashirika haya hayataki kuitikia mualiko wetu wa kuja hapa Tripoli, kuanzisha ofisi zao na kwenda Misrata na kuripoti wakiwa huku huku. Badala yake, wanasikiliza taarifa za kwenye simu na ripoti za waasi tu na kuzichukulia kuwa ndio ukweli. Tumefadhaishwa sana na upotoshaji huu." Amesema Ibrahim.
Naye mtoto wa Gaddafi, Saif al-Islam, amelinganisha taarifa zinazotolewa na vyombo vya habari juu ya vikosi vya serikali kuwalenga raia na taarifa kuhusu kuwepo kwa silaha za maangamizi nchini Iraq, ambazo zilipelekea nchi hiyo kuvamiwa kijeshi.
"Hatujafanya uhalifu wowote ule dhidi ya watu wetu. Nikama lile suala la silaha za maangamizi za Iraq. Mulisema silaha za maangamizi, silaha za maangamizi. Tuishambulie Iraq. Sasa munasema raia wanauawa, raia wanauawa. Tuishambulie Libya." Saif al-Islam ameliambia gazeti la Washington Post.
Hata hivyo, taarifa kutoka Misrata zinathibitisha kutumika kwa mabomu ya mchawanyiko, ambayo yanapotupwa mahala, husambaa kwa haraka katika eneo kubwa zaidi. Dokta Abu Falgha, aliwaonesha waandishi wa habari mabaki ya mabomu hayo.
Kwenye wodi ya wagonjwa wa hospitali ya Misrata, miongoni mwa majeruhi ni mtoto wa miaka 10 anayeitwa Mohammed, ambaye madaktari wanasema alipigwa risasi na mtunguaji. Hakuna uhakika ikiwa Mohammed ataweza kupata fahamu zake kwani, madaktari wanasema, risasi ilimpiga upande mmoja wa kichwa na kutokea mwengine, huku ikiathiri sehemu ya ubongo wake.
Maelfu wakwama Misrata
Kwa upande mwengine, Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM), limeonya kwamba kuna idadi kubwa ya watu ambao wamekwama kwenye mji wa Misrata na ambao wanataka kukimbia, jambo ambalo linalifanya shirika hilo kuzidiwa.
Kiongozi wa operesheni ya shirika hilo nchini Libya, Jeremy Haslam, amesema kwamba meli yao ilipowasili kwa mara ya pili jana kwenye bandari ya mji huo, wimbi kubwa la watu liliivamia kuomba kuokolewa kutoka mji huo uliozingirwa, lakini uwezo wao ni mdogo kuweza kumchukua kila mtu.
Kati ya zaidi ya watu 400,000 waliokwama kwenye mji huo, meli za shirika hilo zinaweza kuondoka na watu 1,000 tu kwa mkupuo mmoja, jambo ambalo Haslam amelifananisha na kuchota tone moja la maji tu kwenye bahari.
Uingereza kutovamia kwa jeshi la ardhini
Kwa upande wa kisiasa, Uingereza imerejea msimamo wake wa kutopeleka vikosi vya majeshi ya ardhini nchini Libya, licha ya kuongezeka kwa mashambulizi na maafa dhidi ya raia.
Waziri Mkuu wa nchi hiyo, David Cameron, amekiambia kituo cha televisheni cha Sky News kwamba hakujakuwa na hoja wala haja ya kuingia Libya.
"Tunachosema ni kuwa, hakuna suala la uvamizi au ukaliaji hapa. Hili si suala la Uingereza kuingiza mkuu wake kwenye ardhi ya Libya, na sisi hatupo hapa kwa ajili hiyo." Amesema Cameron.
Licha ya NATO kuendelea na operesheni yake ya kijeshi nchini Libya, hakuna dalili za mafanikio ya karibu.
Mwandishi: Peter Steffe/ZPR/AFP
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman