Mahusiano ya Ujerumani-Ethiopia yayumba kuhusu Tigray
23 Februari 2021Wakati Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alimpigia simu Waziri Mkuu Abiy Ahmed mapema Februari mwaka huu, alisisitiza kuhusu umuhimu wa kutafuta suluhisho la kufumu kwa mzozo wa Tigray. Merkel pia alisisitiza kuwa raia walionasa katika mapigano lazima wapewe msaada wa kiutu.
Soma zaidi: HRW: Mashambulizi yasababisha vifo vya watu wengi katika siku za mwanzo za vita Tigray
Simu ya Merkel ilikuwa ishara kubwa kabisa ya wasiwasi wa Ujerumani kuhusu mgogoro huo, ijapokuwa mwishoni mwa Novemba, wiki chache tu baada ya mapigano kuanza, Waziri wa Mambo ya Kigeni Heiko Maas alikutana na mwenzake mjini Berlin na kujadili hali ya Tigray. Katika wakati huo, Maas aliyaita mateso ya raia kuwa ya kushutusha na akataka uchunguzi kuhusu uhalifu dhidi ya raia ufanyike na watakaopatikana na hatia wawajibishwe.
Janga la kibinaadamu
Mpaka sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kuutuliza mvutano wa eneo hilo. Kinyume chake ni kuwa hali katika jimbo hilo la mgogoro imeendelea kuwa mbaya. Kilichoanza Novemba 2020 kama uingiliaji wa muda mfupi wa jeshi dhidi ya chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray – TPLF kimebadilika na kuwa mzozo wa kikanda.
Kwa wakati mmoja mambo yalikuwa tofauti, huku Ujerumani ikiongeza urafiki baada ya Abiy kuchaguliwa kuwa kiongozi wa nchi hiyo 2018. Aliwaachia wafungwa wa kisiasa, akaahidi uchaguzi wa huru na akaleta maridhiano na Eritrea. Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Maas na Rais Frank-Walter Steinmeier wakaitembelea nchi yake, Abiy akazuru Berlin
Nchi yake ikaingizwa katika Mpango wa Ushirikiano kati ya Ujerumani na Afrika unaolenga kukuza uwezekaji wa kigeni barani humo.
Msaada wa maendeleo kutumiwa kama mbinu
Sasa, shauku yote imepungua kwa sasa, kwa mujibu wa Annette Weber, mtalaamu wa Ethiopia katika Taasisi ya Kijerumani ya Masuala ya Usalama wa Kimataifa – SWP, Shirika la Msalaba Mwekundu la Ethiopia limeonya kuwa asilimia 80 ya watu wa Tigray hawapati msaada wa kibinaadamu.
Serikali ya Kansela Merkel inaunga mkono juhudi za kidiplomasia za Umoja wa Afrika – AU kupatikana amani. Merkel mwenyewe ametoa wito wa kusitishwa uhasama. Weber anaiambia DW kuwa mataifa ya Magharibi yanakubaliana kuhusu ujumbe unaopaswa kuwasilishwa kwa Abiy. Sauti ya Ujerumani inabeba uzito mkubwa katika muktadha huu.
Weber anasema Ujerumani inaweza pia kutumia msaada wa maendeleo kama mbinu ya kushinikiza kupatikana amani. Ethiopia ni mpokeaji mkubwa wa msaada wa maendeleo kutoka Ujerumani. Mwaka wa 2019, ujerumani ilitoa ahadi mpya ya karibu dola milioni 353 kwa nchi hiyo.
Ethiopia pia ni mmoja wa kile kinachofahamika kama washirika wa mageuzi wa Ujerumani: nchi ambazo Ujerumani inashirikiana nazo hasa kwa karibu kwa sababu zinaonekana kuwa na ajenda halali ya mageuzi.
Umoja wa Ulaya ulijibu mgogoro wa Tigray kwa kusitisha karibu dola bilioni 90 katika malipo ya bajeti ya msaada wake Desemba mwaka jana. Ujerumani inaweza ikachukua hatua sawa na hizo.
Ethiopia inautegemea Umoja wa UIaya
Eva-Maria Schreiber, mbunge wa chama cha Die Linke nchini Ujerumani, anaamini juhudi zite hizi hazitoshi. Mwanasiasa huyo ambaye ni mtalaamu wa masuala ya misaada ya maendeleo anasema serikali ya Ujerumani haipaswi kusitisha ushirikiano wake wa kimaendeleo. Lakini ana mtazamo kuwa inapaswa kuifuta hadhi ya Ethiopia ya kuwa "mshirika wa mageuzi.”
Soma zaidi: UN yaelezea wasiwasi kuhusu hali ya kibinadamu katika eneo la Tigray, Ethiopia
Schreiber anasema nchi inayoorodheshwa kuwa mshirika wa mageuzi lazima iongozwe kidemokrasia na kuheshimu haki za binaadamu, na vigezo hivi havitimizwi chini ya serikali ya Abiy Ahmed.
Schreiber pia anaitaka Ujerumani isitishe ushirikiano wake wa kiuchumi na nchi hiyo ya Afrika. Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo nchini Ujerumani – BMZ inafanya kazi pamoja na Zaidi ya kampuni 100 za Ethiopia katika sekta ya nguo pekee.
Ethiopia, nchi kubwa yenye idadi ya Zaidi ya watu 100, inahitaji kwa dharura msaada wa aina hiyo.
Mchambuzi Weber anasema serikali mjini Addis Ababa haina uwezo wa kuendeleza mipango yake ya maendeleo ya kiuchumi na mnageuzi ya kisiasa bila msaada kutoka Marekani, na juu ya yote Ulaya.
Makala hii awali ilichapishwa katika Kijerumani