1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMamlaka ya Palestina

Makubaliano ya kusitisha vita yaanza Gaza

19 Januari 2025

Makubaliano ya usitishaji vita kati ya Israel na kundi la Hamas,yameanza kutekelezwa muda mfupi uliopita baada ya kucheleweshwa kwa takriban saa tatu.

https://p.dw.com/p/4pL4V
Ukanda wa Gaza 2025 | Wapalestina wakiwa njiani kurejea kabla ya usitishaji mapigano kuanza kutumika
Wapalestina wakiwa njiani kurejea nyumbani baada ya makubaliano ya usitishaji mapigano kuanza.Picha: Dawoud Abu Alkas/REUTERS

Utekelezaji huo umeanza baada ya Kundi la wanamgambo la Hamas kutangaza orodha ya majina matatu ya Waisrael watakaoachiliwa huru.

Mapema leo asubuhi jeshi la Israel liliendelea  kufanya mashambulizi dhidi ya Ukanda wa Gaza likisema, utekelezaji makubaliano hayo umecheleweshwa na Hamas, kwa kutotowa  orodha ya mateka itakaowaachilia.

Soma pia: Israel itawaachilia zaidi ya wafungwa 1900 wa Kipalestina

Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari alitowa taarifa kupitia televisheni,akisema jeshi linaendelea kufanya mashambulizi ndani ya Gaza.

Waziri mkuu Benjamin Netanyahu alitowa maagizo ya kutotekelezwa usitishaji mapigano hadi Hamas itakapotimiza ahadi zake. Shirika la habari la AFP lilionesha video ya mamia ya watu wa Gaza wakishangilia mapema alfajiri katika mji wa Deir el-Balah,muda ambao utekelezaji huo wa kusitisha vita ulitarajiwa kuanza. 

Soma pia: Mahmoud Abbas ataja kuwa tayari kuiongoza Gaza baada ya vita

Lakini muda mfupi baadae moshi mzito ulionekana umetanda Kaskazini Mashariki mwa Gaza. Mwandishi wa habari wa AFP amesema jeshi la Israel limeshambulia Kaskazini mwa Gaza. Tariban watu wanane wameuwawa na wengine wengi wamejeruhiwa kwa mujibu wa timu ya waokoaji wa Gaza.