Makubaliano ya Minsk mashakani
13 Februari 2015Katibu Mkuu wa Shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya (OSCE), Lamberto Zannier, amesema kwamba tangu asubuhi ya leo (Februari 13) kumeshuhudiwa kupamba moto kwa mapigano na uhasama kati ya wanajeshi na waasi wa Ukraine, hali inayotishia kuvunjika kwa makubaliano kabla ya hata muda wa mwisho wa kuweka silaha chini haujafika hapo usiku wa Jumapili ijayo.
"Tayari nimetiwa mashaka na kuendelea kwa uhasama asubuhi hii. Tulitarajia uhasama huu ungelikoma kutokana na masharti ya muda wa mwisho yaliowekwa Minsk. Na tulitazamia sana kuona ukipungua kuanzia sasa. Ni bahati mbaya kwamba kuondosha silaha nzito kwenye uwanja wa mapambano hakumaanishi kulifanya eneo hilo kutokuwa na shughuli za kijeshi."
Mapema, msemaji wa jeshi la Ukraine, Andriy Lysenko, alisema kuwa "adui anaendelea kujimarisha vikosi vyake kwenye maeneo makuu yaliyo kwenye mgogoro", akiongeza kuwa kufikia asubuhi, tayari Ukraine ilishapoteza wanajeshi wake 11 na raia 7, huku wanajeshi wengine 40 wakijeruhiwa.
Makubaliano yaliyofikiwa siku ya Alhamis kwenye mji mkuu wa Belarus, Minsk, yanazipa pande hasimu hadi usiku wa Jumapili ya keshokutwa kuwa zimeshaweka silaha chini na kuelekea kwenye meza ya mazungumzo kwa utatuzi wa kudumu wa mzozo huo ulioanza tangu Aprili mwaka jana, na ambao hadi sasa umeshaangamiza maisha ya watu 5,500.
Kila upande waulaumu mwengine
Lakini, kama yalivyokuwa makubaliano ya awali ya mwezi Septemba kwenye mji huo huo wa Minsk, haya nayo yamekumbana na kikwazo kile kile cha kila upande kutumia fursa ya kuelekea muda wa mwisho kujijengea himaya zaidi kwenye mstari wa mbele wa mapambano, huku kila upande ukiulaumu mwengine.
Kufikia mchana wa Ijumaa, milio ya risasi na makombora ilikuwa ikisikika viunga vya miji ya Donestk na Luhansk huku anga likitandwa na moshi mzito wa majengo yaliyoshambuliwa.
Pamoja na hayo, Urusi, inayotuhumiwa na Ukraine na washirika wake wa Magharibi kuwasaidia waasi wanaotaka kujitenga, imesema inatazamia kuwa pande zote hasimu zitaheshimu makubaliano hayo ya Minsk.
Msemaji wa ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov, alisema: "Makubaliano ya mara hii yaliungwa mkono na viongozi wakubwa na tunatarajia kuwa pande zote zitaheshimu ahadi zao."
Peskov aliongeza kwamba Rais Vladimir Putin wa Urusi, Petro Poroshenko wa Ukraine, Francois Hollande wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani watazungumza kwa njia ya simu, usiku wa Jumamosi.
Ni viongozi hao ambapo hapo jana wakiwa kwenye mji mkuu wa Belarus, Minsk, walifikia makubaliano ya kusitishwa mapigano kwenye eneo la kusini mashariki mwa Ukraine ifikapo tarehe 15 Februari.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga