"Mapungufu ya kisheria": wafanyakazi wa WHO kutowajibishwa
6 Februari 2023Matokeo hayo ni kutokana na kile baadhi ya maafisa wanaelezea kama "mapungufu ya kisheria'' katika jinsi WHO inavyowachukulia waathiriwa wa tabia kama hiyo.
Nakala ya ripoti hiyo ambayo iliwasilishwa mwezi uliyopita kwa Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus na ambayo haikutangazwa hadharani, ilipatikana na shirika la habari cha The Associated Press. Hata hivyo WHO haijaeleza hadharani maudhui ya ripoti hiyo.
Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa unajiri baada ya ukaguzi wa mwaka 2021 uliofanywa na jopo lilioteuliwa na Tedros ambalo liligundua kuwa maafisa watatu wa WHO walipuuza kesi ya utovu wa nidhamu ya ngono iliyoripotiwa kwa mara ya kwanza na shirika la habari la AP mapema mwaka huo, na iliyohusisha daktari wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa kutia saini mkataba wa kununua ardhi kwa binti ambaye aliripotiwa kumpa mimba.
Soma zaidi: WHO yaahidi mabadiliko makubwa
Wiki iliyopita, Tedros alibaini kuwa wachunguzi wa Umoja wa Mataifa walihitimisha kwamba mashtaka hayo hayakuwa na uthibitisho na wafanyakazi watatu waliohusika walirejeshwa kazini baada ya kumalizika likizo yao. Mkuu wa WHO alisema shirika hilo litaomba ushauri kutoka kwa wataalam kuhusu jinsi ya kushughulikia tofauti kati ya ripoti hizo mbili.
Viongozi wa WHO walifahamu matukio hayo bila kuchukua hatua
Kwa upande wao wachunguzi wanasema Tedros aliarifiwa kuhusu madai ya utovu wa nidhamu wa ngono mnamo 2019 na alikuwa ameonywa juu ya mapungufu yanayotia wasiwasi katika sera za utovu wa nidhamu za WHO mwaka uliopita.
Mtaalam wa afya duniani katika Chuo Kikuu cha Columbia Dokta Irwin Redlener amesema ikiwa masuala haya yaliwasilishwa kwa Tedros na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa, basi nchi wanachama wa WHO ni lazima wahimize uwajibikaji kwa hilo.
Soma zaidi: WHO kuzindua uchunguzi wa madai ya ngono DRC
Awali, Tedros alitaja kufahamu juu ya malalamiko ya matendo maovu ya ngono nchini Kongo mara tu baada ya ripoti za vyombo vya habari mnamo Septemba 2020. Alisema mtu yeyote anayehusishwa na makosa ya kijinsia atakabiliwa na madhara ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi. Lakini hadi sasa, hakuna wafanyakazi wakuu wa WHO wanaohusishwa na unyanyasaji na unyonyaji ambao wamefutwa kazi.
Mnamo Mei 2021, uchunguzi wa AP ulifichua kuwa usimamizi mkuu wa WHO ulifahamishwa juu ya unyanyasaji wa kijinsia wakati wa juhudi za kukomesha ugonjwa wa Ebola mashariki mwa Kongo kuanzia mwaka 2018-2020, lakini shirika hilo halikufanya chochote kuizuia vitendo hivyo.
Daktari wa WHO atajwa kuhusika katika vitendo hivyo
Shirika la habari la AP lilichapisha makubaliano yaliyothibitishwa kati ya daktari wa zamani wa WHO Jean-Paul Ngandu na mwanamke anayedaiwa kumpa ujauzito, ambapo daktari huyo alikubali kugharamia huduma ya afya na kumnunulia eneo la ardhi. Makubaliano hayo yalitiwa pia saini na wafanyakazi wawili wa WHO, kwa lengo la kulinda heshima ya WHO. Kulingana na mawasiliano ya ndani ya WHO, mwanamke huyo na shangazi yake walikwenda katika ofisi za WHO huko Beni kutoa malalamiko kuhusu Daktari Ngandu.
Soma zaidi: Umoja wa Mataifa hatiani kuhusu unyanyasaji wa kingono DRC
Tathmini imeeleza kuwa uamuzi huo ulifanywa na maafisa wa sheria na maadili kutoka shirika la afya la Umoja wa Mataifa pamoja na idara nyingine ulikuwa
wazi kwamba mwanamke huyo hakuwa "mnufaika'' wa usaidizi wa WHO wala hakupokea msaada wa kibinaadamu kutoka kwa wakala wa shirika hilo, na hivyo, hatambuliwi kama mwathirika chini ya sera za WHO.
Wafanyakazi wa WHO waliohojiwa na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamesema hii inaweza kuchukuliwa kama "mapungufu ya kisheria" ambayo yanaweza kusababisha malalamiko kama haya kutoshughulikiwa.