Marekani kuitaja Kenya "mshirika wake mkuu" wa nje ya NATO
23 Mei 2024Rais Ruto yuko ziarani nchini Marekani kwa siku tatu.
Biden, pamoja na mambo mengine, anatarajiwa kulitaja taifa hilo la Afrika Mashariki ambalo si mwanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO kuwa mshirika wake mkuu, wakati Kenya ikijiandaa kupeleka vikosi nchini Haiti kama sehemu ya juhudi zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa kushughulikia mzozo wa usalama nchini humo.
Kenya linakuwa taifa la kwanza la kusini mwa jangwa la Sahara kupewa hadhi hiyo, hatua inayoakisi mkakati wa Washington wa kuimarisha ushirikiano na taifa hilo la Afrika Mashariki, ambalo kwa muda mrefu limekuwa na uhusiano wa karibu mno na wapinzani wakubwa wa Marekani, China na Urusi.
Kenya inatarajia kupeleka kama polisi 1,000 nchini Haiti watakaokuwa sehemu ya ujumbe wa wa kuimarisha hali ya usalama katikati ya ongezeko la machafuko yanayosababishwa na mapigano baina ya magenge ya uhalifu.
Mataifa mengine yanayotarajiwa kusaidiana na Kenya ni Bahamas, Barbados, Benin, Chad na Bangladesh.
Uamuzi wa Ruto kutuma vikosi vya polisi nchini Haiti ulikaribishwa na Rais Biden aliyesema Marekani "itawajibika kikamilifu kuisaidia Kenya katika mpango huo.
Wakuu hao aidha walijadiliana juu ya kuimarisha uhusiano katika fursa za uwekezaji na hususan kwenye eneo la teknolojia, na kumtolea wito Rais Rutto kuangazia fursa zaidi za kuimarisha uhusiano huo.
"Tunaomba mtusaidie kupata fursa ya kuzileta pamoja sekta ya umma na binafsi. Na tunahitaji mtusaidie kuimarisha ugavi katika viwanda kwa siku zijazo, ikiwa ni pamoja na nishati safi na biashara ya mtandaoni pia."
Biden amesema sasa wanazindua enzi mpya ya ushirikiano wa kiteknolojia kati ya Kenya na Marekani, ikiwa ni pamoja na ubadilishanaji mpya na uwekezaji katika nyanja muhimu za usalama wa mtandao, akili ya kubuni na mengineyo.
Kwa upande wake Rais William Ruto alisema idadi ya vijana wa Kenya wenye vipaji na wasomi lakini pia wabunifu inaendana sambamba na ukuaji wa teknolojia, mitaji na wawekezaji nchini Marekani.
Soma pia:Kenya inatafuta utulivu wa kiuchumi baada ya miaka 60 ya uhuru
Ruto aidha amekutana na Spika wa bunge la Marekani Mike Johnson kwenye jengo la Bunge, Capitol Hill na kumwambia ataitumia ziara hiyo kama sehemu ya kushirikishana masuala yanayoibua wasiwasi kutokana na changamoto zilizosababishwa na mzigo wa madeni nchini Kenya na kote barani Afrika.
Marekani na Kenya zinaadhimisha miaka 60 ya mahusiano ya kidiplomasia. Kesho Ijumaa, Ruto anatazamiwa kushiriki hafla ya Baraza la Wafanyabiashara la Marekani, sambamba na Makamu Rais Kamala Harris.