Mashambulizi ya wapiganaji yawahamisha maelfu Msumbiji
28 Februari 2024Akizungumza na waandishi wa habari katika mji mkuu Maputo, msemaji wa serikali Filimao Suaze amesema takriban watu 67,321 wamekimbia maakazi yao akielezea hali katika jimbo la Cabo Delgado na kuongezea kwamba Idadi hii inalingana na familia 14,270 ambazo zinadhaniwa kuwa zimefika katika mkoa wa Nampula na maeneo mengine.
Suaze hata hivyo amesema serikali "haiamini kwamba hali ya Cabo Delgado imefikia masharti ya kutangaza hali ya hatari."
Kulingana na ripoti za ndani na takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM, Machafuko mapya yalizuka kaskazini mwa Msumbiji wiki mbili zilizopita.
Mwandishi wa habari wa AFP ameripoti kuwaona, maelfu ya watu waliokimbia makazi yao wakitembea kwenye mvua, wengine wakiwa wamebeba magunia ya nguo na watoto wachanga mgongoni.
Huku wengine wakisimama kwenye changarawe walipokuwa wakisubiri vifurushi vya chakula vilivyogawanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP.
oma pia: Mapigano mapya Msumbiji yasababisha maelfu kuyakimbia makaazi yao
IOM imetaja idadi ya waliokimbia mashambulizi kutoka Macomia, Chiure, Mecufi, Mocimboa da Praia na Muidumbe kuwa 71,681 kati ya Desemba 22 na Februari 25.
Kati ya Jumatano iliyopita na Alhamisi pekee IOM ilirekodi zaidi ya watu 30,000 waliokimbia makazi yao waliowasili katika mji wa Namapa, katika jimbo la Nampula, kwa basi, boti au kwa miguu.
Mendes Luciano baba wa watoto wawili mwenye umri wa miaka 23 ni miongoni mwa waliokimbia makaazi yao, aliiambia AFP kuhusu "mateso", waliopitia akiongeza kuwa "hawajala chochote" tangu walipowasili wiki iliyopita.
Msemaji wa IOM amesema mahitaji ya kimsingi yanayotolewa katika wilaya zote ni pamoja na chakula, malazi, huduma za afya na usaidizi.
Soma pia: Marekani: Tutaisaidia Msumbiji kupambana na uasi
Uasi nchini Msumbuji ulianza Oktoba 2017 wakati wapiganaji hao waliojitangaza kuwa wanashirikiana na kundi linalojiita Dola la Kiislam waliposhambulia maeneo ya pwani ya kaskazini mwa Cabo Delgado yenye utajiri wa gesi, karibu na mpaka wa Tanzania.
Tangu Julai 2021, maelfu ya wanajeshi kutoka Rwanda na kutoka jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC wamepelekwa kushirikiana na jeshi la Msumbiji na tangu wakati huo wamesaidia kutwaa tena udhibiti wa sehemu kubwa ya Cabo Delgado.
Ujumbe wa SADC utakamilisha operesheni yake katikati ya Julai kulingana na kambiyo, lakini msemaji wa serikali ya Msumbiji Filimao Suaze amekataa kuzungumzia hatua hiyo angalau kwa sasa.
Soma pia: Makovu ya mashambulizi ya wanamgambo Msumbiji
Suaze amesisitiza kwamba Msumbiji "inafanya kila iwezalo" "kupambana na ugaidi na kuhakikisha usalama kwa idadi ya watu katika kiwango ambacho hata kama kikosi fulani kiliondoka au kingine kubaki sio muhimu". akiongeza kwamba "Serikali iko makini."
Wiki iliyopita Rais Filipe Nyusi alithibitisha harakati mpya za uasi, lakini alipuuza tishio hilo na kusisitiza kuwa vikosi vya usalama vinadhibiti hali hiyo.
Takriban watu 5,000 wameuawa na karibu milioni moja wamelazimika kukimbia makazi yao tangu wanamgambo wanaohusishwa na IS kuanzisha uasi.