Mji wa Bor, Sudan Kusini wadhibitiwa na wanajeshi waasi
19 Desemba 2013Mapigano hayo makali yanatishia kuitumbukiza nchi hiyo kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Msemaji wa Jeshi la Sudan Kusini, Kanali Philip Aguer, amesema leo (19.12.2013) kuwa wanajeshi waasi wanaomtii aliyekuwa makamu wa Rais wa nchi hiyo Riek Machar wameutwaa mji wa Bor.
Amesema viongozi katika mji huo ambao ni mji mkuu wa jimbo la Jonglei, hawapokei simu zao, hatua inayoifanya serikali kuu kuamini kwamba wamejiunga na waasi.
Kanali Aguer amesema wamepoteza udhibiti wa mji wa Bor na kwamba milio ya risasi imesikika usiku kucha ingawa bado hawana taarifa kuhusu waathirika au watu walioyakimbia makaazi yao kwa sababu operesheni za kijeshi bado zinaendelea.
Watu 19 wauawa Bor
Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Martin Nesirky amesema raia 19 wameuawa katika mji wa Bor, akifafanua kuwa taarifa hizo zimetolewa na shirika la Msalaba Mwekundu nchini Sudan Kusini.
Amesema wasiwasi pia umeongezeka katika majimbo ya Unity na Upper Nile na mji wa Torit na mapigano yamesambaa katika miji mingine ya taifa hilo tajiri kwa mafuta.
Waziri wa Habari wa Sudan Kusini, Michael Makuei Lueth, amesema kiasi watu 500, wengi wao wakiwa wanajeshi, wameuawa na wengine 700 wamejeruhiwa katika mapigano hayo yaliyoanza wakati wa jaribio la mapinduzi mwishoni mwa wiki iliyopita.
Rais Salva Kiir amesema yuko tayari kuanza mazungumzo na makamu wake aliyemfukuza kazi mwezi Julai, Riek Machar. Kiir anamlaumu Machar kuhusika na jaribio la mapinduzi lililoshindwa na kwa kuanzisha mapigano. Hata hivyo, Machar amekanusha madai hayo.
IGAD na juhudi za kumaliza mapigano
Wakati huo huo mawaziri wa mambo ya nje kutoka mataifa manne ya Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Mashariki na Pembe ya Afrika-IGAD, wameelekea Sudan Kusini kuanza juhudi za kumaliza mapigano hayo yanayozusha hofu ya kugeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mawaziri hao wanatokea Kenya, Djibouti, Ethiopia na Uganda.
Kwa upande wake Marekani imeelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu mapigano ya Sudan Kusini, huku Waziri wake wa mambo ya nje, John Kerry akitoa wito wa kuwepo utulivu. Marekani na Uingereza zimeanza kuwaondoa wafanyakazi wake kutoka Juba.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon alisema jana Jumatano (18.12.2013) kuwa Sudan Kusini inakabiliwa na mzozo wa kisiasa ambao unaweza ukasambaa zaidi na unatishia kuitumbukiza nchi hiyo kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Maelfu ya raia wa Sudan Kusini wameyakimbia makaazi yao na kwenda kutafuta hifadhi kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa tangu yalipozuka mapigano siku ya Jumapili.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,RTRE,AFPE
Mhariri: Ssessanga Iddi