Mkutano wa kilele kati ya Urusi na Afrika wafunguliwa rasmi
27 Julai 2023Rais wa Urusi Vladimir Putin anawapokea leo Alhamisi viongozi wa nchi za Afrika kwa ajili ya mkutano wa kilele katika mji wa Saint Petersburg, wakati bara hilo likikabiliana na matokeo ya Moscow kujiondoa katika mkataba wa kimataifa wa usafirishaji nafaka za Ukraine.
Kusitishwa kwa mkataba huo ambao uliwezesha mauzo ya nafaka za Ukraine kupitia Bahari Nyeusi hadi katika masoko ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Afrika, unatarajiwa kutawala ajenda za mkutano huo.
Makubaliano hayo yalipelekea karibu tani milioni 33 za nafaka kuondoka kwenye bandari za Ukraine, na kusaidia kuleta utulivu wa bei ya chakula duniani na kuepusha uhaba wa nafaka na bidhaa nyingine muhimu.
Soma pia: Urusi kuchukuwa nafasi ya Ukraine kupeleka ngano Afrika - Putin
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amewatolea wito viongozi wa Afrika watakaohudhuria mkutano huo, kudai majibu kuhusu usumbufu wa nafaka ambao umesababisha mataifa maskini zaidi kuelekea kwenye mgogoro wa chakula. Aidha Blinken amesema:
" Matarajio yangu ni kwamba Urusi itasikia vyema ombi hili kutoka kwa washirika wetu wa Kiafrika watakapokutana."
Putin ambaye ametengwa kimataifa tangu kuanzisha uvamizi wa kijeshi nchini Ukraine, bado anaungwa mkono katika nchi kadhaa za Kiafrika.
Kuandaa mkutano huo na viongozi wa bara la Afrika, Rais Putin analenga kuonyesha kwamba hajatengwa kimataifa licha ya vita vinavyoendelea, na pia ana nia ya kuendelea majadiliano juu ya mpango wa amani unaohusisha mataifa ya Afrika ili kutafutia suluhu mzozo wa Ukraine.
Soma pia: Putin akutana na viongozi wa Afrika
Katika barua ya kuwakaribisha washiriki wa mkutano huo, Putin amesema ni muhimu kuona katika miaka ya hivi karibuni ushirikiano na Afrika umefikia kiwango kipya na wananuia kuuendeleza zaidi.
Mbali na usalama wa chakula, mkutano huo unatarajiwa kushughulikia suala la kukuza biashara hasa ikizingatiwa kuwa Urusi ni muuzaji mkubwa
wa silaha barani Afrika. Putin anatarajiwa kufanya mazungumzo ya pande mbili na marais wa Afrika na anatarajiwa kutoa hotuba wakati wa mkutano huo.
Mkutano huu ni wa pili na unafanyika leo na kesho Ijumaa na utahudhuriwa na wawakilishi 49 kati ya 54 kutoka mataifa ya kiafrika huku 17 wakiwa wakuu wa nchi akiwemo Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.
Soma pia: Urusi inataka nini Afrika?
Ni idadi ndogo kuliko wakati wa mkutano wa kilele wa uzinduzi mnamo mwaka 2019 huko Sochi, kusini mwa Urusi. Ikulu ya Urusi Kremlin imezishutumu nchi za Magharibi kwa kujaribu kuyazuia mataifa ya Afrika kushiriki katika mkutano huo.
Kulingana na mshauri wa sera za kigeni wa Ikulu ya Kremlin Yuri Ushakov, katika hotuba yake, Putin atazungumzia mtazamo wake juu ya uhusiano kati ya Urusi na Afrika na kuundwa kwa utaratibu mpya wa dunia.