Mkutano wa miundombinu waanza leo China
17 Oktoba 2023Hata hivyo macho na masikio yataelekezwa pia kwa Rais wa Urusi Vladmir Putin ambaye ameshawasili nchini humo akitafuta kukuza uhusiano wake na Beijing. Mkusanyiko huo unawaleta pamoja wawakilishi kutoka masoko yanayoendelea kusini mashariki mwa Asia, Asia kusini, mashariki ya kati na Amerika ya kusini.
Rais Vladmir Putin anahudhuria mkutano huo ikiwa ni mara ya kwanza kutembelea taifa kubwa tangu mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC ilipotoa waranti wa kumkamata mnamo mwezi Machi baada ya Urusi kuivamia Ukraine. Kwenye ziara hiyo, Putin anatarajiwa kuiomba China kuiunga mkono Urusi kiuchumi na kidiplomasia. Urusi imekuwa ikilenga kuelekeza shughuli zake za kibiashara barani Asia baada ya kufungiwa na Umoja wa Ulaýa kutokana na mzozo wa Ukraine.
Soma zaidi: Putin kukutana na Jinping
Chini ya mradi huo wa miundombinu, makampuni ya China yameshajenga bandari, barabara, reli, vinu vya kuzalisha nishati na miundo mbinu mingine kote duniani ili kukuza biashara na ukuaji wa uchumi. Hata hivyo madeni makubwa yaliyotokana na mikopo ya Beijing ya ufadhili wa miradi hiyo yamekuwa yakikosolewa kuwa ni mzigo kwa nchi masikini.
Sri Lanka na Zambia ni miongoni mwa mataifa ambayo yameelemewa na madeni ya China na wakopeshaji wengine wa kimataifa. Rais wa zamani wa Sri Lanka Gotabaya Rajapaksa, alijiuzulu mwezi Julai mwaka 2022 katikati ya maandamano makubwa ya kupinga mfumuko mkubwa wa bei na mgogoro mkubwa wa kiuchumi. China iliikopesha Sri Lanka kuiwezesha kujenga barabara kubwa, bandari uwanja wa ndege na kusababisha deni la dola za kimarekani bilioni 7.
Kabla ya kuanza kwa mkutano wa leo Rais wa China Xi Jin Ping amekutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ambapo wametia saini makubaliano ya kuanzisha ushirikiano. Hatua hiyo ya China ya kukuza uhusiano wake na Ethiopia ni ishara ya kuonesha kuiunga mkono wakati Beijing ikiendeleza juhudi za kuimarisha ushawishi barani Afrika.
Rais wa Kenya, William Ruto ni mmoja wa wakuu wa nchi wanaohudhuria mkutano huo nchi yake ikiwa na moja ya miradi muhimu iliyojengwa kupitia sera hiyo ya miundo mbinu ya China. Mradi huo ni wa barabara yenye Kilometa 592 kutoka Mombasa kuelekea Nairobi na inaunganisha bandari kubwa ya Kenya na mji mkuu. Ulianzishwa mwaka 2017 na China inauchukulia mradi huo kama moja ya mafanikio makubwa
Vyanzo: AP/Reuters