1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa NATO wazongwa na mivutano

Daniel Gakuba
4 Desemba 2019

Siku ya kwanza ya mkutano wa wakuu wa nchi za Umoja wa Kujihami wa NATO ilishuhudia kubadilishana maneno makali kati ya Raimarais Donald Trump na Emmanuel Macron, na matakwa ya Uturuki yanayotishia kusababisha mkwamo.

https://p.dw.com/p/3UBTx
London NATO-Gipfel Macron und Trump
Picha: Reuters/L. Marin

Hafla ya kuadhimisha miaka 70 tangu kuundwa kwa jumuiya hiyo ya ushirikiano wa kijeshi kati ya Ulaya na Amerika Kaskazini, NATO ilianzia katika makao makuu ya Malkia wa Uingereza Elisabeth II, na kisha kuendelea nyumbani kwa waziri mkuu Boris Johnson, namba 10 katika mtaa wa Downing. Yalikuwa mapokezi rahisi, ambapo viongozi hao walikarimiwa kwa glasi chache za vinywaji, huku wakiwa wamesimama.

Matukio makubwa kwa siku hiyo yalikuwa ubadilishanaji wa maneno makali kati ya marais Donald Trump wa Marekani na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron. Kwanza Trump alimshambulia Macron, kwa kusema kauli yake ya awali kwamba NATO ilikuwa imekufa kimawazo, ilikuwa chafu na yenye dharau, na kuongeza kuwa Ufaransa ni nchi inayohitaji ulinzi wa NATO kuliko nchi nyingine.

Macron amtaka Trump kuacha mzaha

Lakini viongozi hao wawili walipokaa pamoja, Trump alipunguza makali ya lugha, badala yake alizungumza kwa utani, akimuuliza Macron ikiwa Ufaransa ingependelea kuwapokea magaidi wote waliokamatwa nchini Syria. Rais Macron hakufurahia utani huo, na kwa ukali alisema, ''hebu tuache mambo ya mzaha''.

UK Nato-Gipfel
Picha ya pamoja ya viongozi wa nchi wanachama wa NATOPicha: picture-alliance/AP Photo/Yui Mok

Chanzo kingine cha mvutano katika mkutano huo, ni hatua za Uturuki za kununua mfumo wa ulinzi wa makombora kutoka Urusi, na sharti la kutaka NATO iliweke kundi la Wakurdi la YPG kwenye orodha yake ya magaidi, sharti ambalo baadhi ya wanachama kama Ufaransa hazilikubali, ikizingatiwa kuwa kundi hilo lilikuwa mshirika mkubwa wa NATO katika vita dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

China yatambuliwa kama taifa kubwa, lenye kitisho

Brüssel PK Jens Stoltenberg NATO Generalsekretär
Katibu Mkuu wa NATO, Jens StoltenbergPicha: Reuters/F. Lenoir

Kwa mara ya kwanza, NATO imeizungumzia China katika tangazo la pamoja la viongozi, ikiitambua kama taifa kubwa ambalo ushawishi wake unaozidi kupanuka unaambatana na fursa pamoja na changamoto kwa wanachama wote wa jumuiya hiyo. Hili nalo huenda lisipate muafaka wa wanachama wote, kwani nchi muhimu kama Ujerumani zinapendelea kuwa na sera binafsi kuhusu mahusiano yake na China.

Shinikizo la Rais Donald Trump kuzitanka nchi nyingine zitoe fedha zaidi kugharimia uendeshaji wa shughuli za NATO halikuepukika, ingawa halikupata muda wa kutosha katika mkutano wa saa tatu tu.

Katika hali hii ya mvutano, katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wanatazamiwa kutumia maarifa yao ya kidiplomasia, kutafuta suluhu.

 

Barbara Wesel