Mzozo waibuka kati ya Sudan na Umoja wa Falme za Kiarabu
22 Desemba 2023Mnamo mwezi November, Jenerali Yasser Al-Atta, naibu wa mkuu wa majeshi Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan, aliulaani wazi wazi Umoja wa Falme za Kiarabu na kuuita taifa la mafia ambalo limechukua njia ya uovu kwa kuliunga mkono kundi la RSF na kiongozi wake Mohamed Hamdan Daglo.
Atta aliishtumu Abu Dhabi kusafirisha silaha kupitia Chad, Uganda na Jmahuri ya Afrika ya Kati kwenda kwa RSF kwa msaada wa kundi la mamluki wa Urusi la Wagner, ambalo wakati mmoja lilikuwa na ushawishi mkubwa kwa serikali mjini Bangui.
Soma pia: UN: Zaidi ya watu milioni 7 wamekimbia mapigano Sudan
Baada ya kudhoofika kwa Wagner, ndege zao pia zimepitia Chad, na kutua kwa wiki katika uwanja wa ndege wa N'Djemena, aliongeza Atta na kumshutumu pia jenerali wa mashariki mwa Libya Khalifa Haftar kuwa msambazaji wa vifaa vya kijeshi kwa RSF.
Maafisa wa UAE hawakujibu ombi la kuzungumzia shutuma hizo. Wataalamu walionya juu ya kuwepo kwa njia hiyo ya usambazaji tangu kuanza kwa vita, lakini hadi Novemba jeshi la Sudan lilikuwa halijatoa shutuma hizo hadharani.
Jalel Harchaoui, mchambuzi kutoka Royal United Services Institute (RUSI), alisema hadi hivi karibuni, kambi ya Burhan ilitumia tahadhari na diplomasia, ili kuepuka malumbano ya moja kwa moja ya maneno dhidi ya wahusika wakuu kama vile Haftar wa Libya, Urusi na Abu Dhabi.
Lakini jeshi limetupilia mbali tahadhari hiyo kwa kuweka hadharani shtuma zake na kuitaka wizara ya mambo ya nje kuwafukuza wanadiplomasia 15 wa UAE.
Mnamo mwezi Agosti, Jarida la Wall Street Journal liliripoti kuwa shehena za misaada zilizotumwa kupitia Uganda kwa ajili ya wakimbizi wa Sudan nchini Chad zilibainika kuwa na silaha zinazopelekwa kwa RSF. UAE ilikanusha ripoti hiyo mara moja, na ksuema Abu Dhabi haiegemei upande wowote katika mzozo wa sasa.
Soma pia: UAE yakanusha kutuma silaha Sudan
Mtaalamu wa Sudan Alex de Waal, alisema Rais wa UAE Mohamed bin Zayed alikuwa muungaji mkono wa mkuu wa RSF Daglo.
De Waal alisema wawili hao walijenga uhusiano mwaka 2015 wakati Daglo alipotoa wapiganaji kwa ajili ya ardhini ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen.
Naye profesa wa masuala ya usalama katika chuo cha King's College mjini London, Andreas Krieg, alisema hadithi ya UAE nchini Sudan ni mmoja ya mitandao inayoratibiwa na Abu Dhabi kufikia malengo yake ya kimkakati kwa ukanushaji wa kuaminika na tahadhari.
Harchaoui wa RUSI, alisema ukanushaji umehakikisha kwamba ukosoaji wowote wa uingiliaji wa Emarati haupati nguvu.
Jeshi lavunja ukimya
Hata hivyo, wakati uvumi ukiendelea kwa miezi kadhaa, mvutano uliibuka mwezi Novemba wakati mamia ya waandamanaji wanaoliunga mkono jeshi walipoingia barabarani katika mji wa mashariki wa Port Sudan wakitaka balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu atimuliwe.
Muda mfupi baadaye, kaimu waziri wa mambo ya nje wa Sudan Ali al-Sadiq alisema Abu Dhabi imewafukuza wanadiplomasia wa Sudan kutoka UAE.
Soma pia:Sudan yasema serikali ya mpito haina mamlaka ya kurejesha mahusiano na Israel
Waziri al-Sadiq aliiambia televisheni ya taifa mapema mwezi huu, kwamba hawakutaka maelezo kutoka UAE ingawa walikuwa na taarifa juu ya ushiriki wao katika vita, na kuongeza kuwa wao, UAE, ndiyo waliowafukuza wanadiplomasia wao na hivyo walilaazimika kujibu.
Wiki iliyopita, wizara ya mambo ya nje ilitangaza wanadiplomasia 15 wa UAE kuwa watu wasiotakiwa, na kuwataka kuondoka Sudan ndani ya saa 48.
Wakati hakuna upande wowote ulioweza kupata ushindi wowote mkubwa wa kijeshi, RSF sasa inadhibiti mitaa ya mji mkuu Khartoum, eneo kubwa la magharibi mwa Darfur, na inazidi kuelekea kusini.
Harchaoui anasema kwa kuchukuwa msimamo mkali zaidi, Burhan huenda anatumai kuvutia nadhari zaidi na ukosoaji wa UAE kwa utoaji haramu wa silaha kwa ajili ya Daglo.