NATO: Hakuna ishara ya uchokozi wa Urusi dhidi ya Romania
7 Septemba 2023Stoltenberg amesema, Jumuiya hiyo haina taarifa zozote zinazoashiria kuwa mabaki ya ndege isiyo na rubani yaliyopatikana katika himaya ya Romania yalisababishwa na shambulio la kukusudia lililofanywa na Urusi dhidi ya taifa hilo.
Soma pia: Urusi yaishambulia upya Ukraine kwa kulenga Bandari zake muhimu
Stoltenberg ameyaeleza hayo mapema leo wakati alizungumza na wabunge wa Umoja wa Ulaya ambapo amesema kwamba, wanasubiri matokeo ya uchunguzi unaoendelea.
Jana Jumatano, waziri wa ulinzi wa Romania Angel Tilvar alisema kuwa mabaki ya vipande vya droni vinavyosadikika kuwa vilitokana na mashambulizi ya Urusi dhidi ya bandari ya mto Danube yamepatikana katika sehemu ya nchi yake ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO tangu mwaka 2004.
Hivi karibuni, kumekuwa na mfululizo wa mashambulizi ya Urusi dhidi ya bandari za mto Danube nchini Ukraine ambazo ziko karibu na Romania.