1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO kutangaza njia za kujibu kitisho cha Urusi

5 Septemba 2014

Viongozi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, wanatarajiwa kutangaza njia za kukabiliana na kitisho kinachosababishwa na Urusi dhidi ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo za Ulaya ya Mashariki.

https://p.dw.com/p/1D7a5
Viongozi wa NATO wanaohudhuria mkutano wa Wales
Viongozi wa NATO wanaohudhuria mkutano wa WalesPicha: picture-alliance/dpa/Maurizio Gambarini

Viongozi hao wanatarajiwa kutangaza msimamo wao kuhusu iwapo watapeleka kikosi kipya cha wanajeshi zaidi pamoja na vifaru Ulaya ya Mashariki, eneo ambalo lina hofu huenda likashambuliwa na Urusi kutokana na uchokozi uliofanywa na nchi hiyo mashariki mwa Ukraine, pamoja na kushinikiza vikwazo vipya dhidi ya Urusi.

Akizungumza leo katika siku ya pili na ya mwisho ya mkutano wa kilele wa NATO unaofanyika Newport, Wales, Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen amesema jumuiya hiyo itaimarisha ushirikiano wake na jumuiya ya kimataifa pamoja na washarika wake ulimwenguni kote.

Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen
Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh RasmussenPicha: Reuters/Yves Herman

Amesema wataendelea kushirikiana kwa karibu kabisa wakati wa amani, ili waweze kupambana kwa pamoja nyakati za mizozo.

Amesema watawasaidia washirika wa NATO kuimarisha sekta yao ya kijeshi na usalama kama watahitaji msaada na kwa wale walio tayari na wana uwezo wa kushiriki katika majukumu ya jumuiya hiyo na wanakidhi masharti ya kuwa mwanachama, milango itaendelea kuachwa wazi.

Ukraine yatarajia kusaini mkataba wa kusitisha vita

Hayo yanajiri wakati ambapo Ukraine inatarajia kusaini mkataba wa kusitisha mapigano mashariki mwa Ukraine, unaoungwa mkono na Urusi, katika mkutano unaofanyika leo kwenye mji mkuu wa Belarus, Minsk.

Hata hivyo, saa chache kabla ya kuanza mazungumzo hayo ya amani yatakayohudhuriwa na wawakilishi wa Ukraine, Urusi, waasi wanaotaka kujitenga pamoja na wajumbe wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya-OSCE, mashambulizi mapya yamefanyika leo kwenye mji wa bandari wa Mariupol.

Kikosi cha jeshi kikiwa Kramatorsk
Kikosi cha jeshi kikiwa KramatorskPicha: Reuters/G.Garanich

Aidha, mashambulizi mengine yamefanyika jana usiku kwenye mji wa waasi wa Donetsk, na hivyo kuweka mashaka ya kufikiwa kwa mpango wa amani uliopendekezwa na Rais wa Urusi, Vladmir Putin. Rais Petro Poroshenko wa Ukraine, amesema ana matumaini makubwa ya kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Uingereza yailaani vikali IS

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, amewataka washirika wa NATO kutolipa fedha kwa ajili ya kuachiwa huru kwa raia wao wanaoshikiliwa mateka na kundi lenye itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu-IS, ambalo linaendesha mashambulizi nchini Iraq na Syria.

Kundi la Dola la Kiislamu linamshikilia mateka raia wa Uingereza na limetishia kumuuwa, licha ya kuwepo taarifa za kuachiwa huru raia wa Ufaransa na Italia, baada ya nchi hizo kulipa kiasi kadhaa cha pesa.

Rais Petro Poroshenko na Rais Vladmir Putin
Rais Petro Poroshenko na Rais Vladmir PutinPicha: CHRISTOPHE ENA/AFP/Getty Images

Cameron amesema jana usiku walizungumzia kitisho kinachowekwa na IS nchini Iraq na Syria na kwamba ujumbe wao uko wazi kabisa kwani wameungana pamoja kulaani vitendo vya kikatili na kudharauliwa.

Mbali na Cameron, viongozi wengine wa mataifa ya Magharibi wanaohudhuria mkutano wa NATO ambao unatajwa kuwa muhimu zaidi tangu enzi ya Vita Baridi, ni pamoja na Rais Barack Obama wa Marekani, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, Rais wa Ufaransa, Francois Hollande na Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Renzi, ambapo wanatarajiwa kukubaliana kusaidia usalama wa Iraq katika kupambana na IS.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE,APE
Mhariri:Josephat Charo