1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi tajiri zalaumiwa kwa kitisho cha kimazingira

28 Mei 2024

Mataifa madogo ya visiwa yanayoendelea yamezitolea wito nchi tajiri zitoe fedha zaidi kuzisaidia kukabiliana na kitisho cha mabadiliko ya tabia nchi.

https://p.dw.com/p/4gN0f
Nchi ndogo za visiwa ziko katika kitisho kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi
Nchi ndogo za visiwa ziko katika kitisho kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchiPicha: Wire Stock/Pond5 Images/IMAGO

Nchi ndogo za visiwa ambazo zinakabiliwa na kitisho kikubwa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, na ambazo hazina utajiri wa kupambana na mabadiliko hayo zenyewe, wala si masikini vya kutosha kutimiza vigezo vya kupewa misaada ya maendeleo na kifedha, zimeyanyoshea kidole cha lawama mataifa tajiri kwa masaibu yao.

Waziri Mkuu wa Antigua na Barbuda, Gaston Browne amesema nchi ndogo za visiwa zinajikuta katika mapambano dhidi ya migogoro iliyoungana. Mzozo unaotakiwa kushughulikiwa kwa dharura kwa sasa ni janga la kimazingira linalozidi kuwa baya huku dunia ikikaribia kiwango cha ongezeko la joto la nyuzi 1.5 katika kipimo cha Celcius, kiwango cha juu kilichowekwa katika mkataba wa mazingira wa Paris.

Waziri Mkuu Browne ameongeza kusema kwamba wachangiaji wakubwa wa mabadiliko ya tabia nchi wameshindwa kutimiza ahadi zao kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, na hivyo kusababisha athari za kuonekana katika nchi ndogo za visiwa na sayari ya dunia kwa ujumla wake.

Mkutano huo wa kimataifa wa nchi ndogo za visiwa zinazoendelea unafanyika mwaka huu katika nchi ya Antigua na Barbuda na unahudhuriwa na nchi takriban 100, ikiwemo Japan. Mkutano huu hufanyika mara moja katika kipindi cha muongo mmoja.

Soma zaidi: Guterres aonya kuhusu ongezeko la joto duniani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameyaeleza mabadiliko ya tabia nchi kama kitisho halisi kwa uhai wa binadamu. "Mabadiliko ya tabia ya nchi ni janga ambalo lipo na linaloikabili familia nzima ya binadamu. Lakini nchi ndogo za visiwa ziko katika msitari wa mbele katika kukabiliwa na hatari kubwa zaidi."

Jumuiya ya kimataifa ina wajibu kuzisaidia nchi za visiwa

Guterres pia amesisitiza kwamba jumuiya ya kimataifa ina wajibu wa kuyasaidia mataifa hayo. Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia amesema wazo kwamba nchi nzima ya kisiwa inaweza kuhabiriwa kutokana na shughuli za sekta ya nishati ya nchi ya ardhi au mashindano kati ya dola kubwa zilizostawi kiuchumi, ni jambo la kutamausha.

Rais wa visiwa vya Marshall Hilda Heine amesema gharama zitaongezeka na zitalipwa zaidi na zaidi kwa maisha ya binadamu ikiwa tutashindwa kukabiliana na chanzo halisi, ambacho ni nishati ya mafuta yanayopatikana chini ya ardhi.

Waziri Mkuu wa taifa huru la Samoa, Fiame Naomi Mata'afa, amezihimiza nchi zilizoendelea kiviwanda zitoe fedha zaidi na aina nyingine ya msaada. Waziri Mkuu huyo aidha amesema mustakhbali wao unaonekana uko hatarini, kima cha maji baharini kinaoengezeka, madeni yanaongezeka na watu wanang'ang'ana.

Mada kuu katika ajenda ya nchi 39 za visiwa, ambazo idadi yao jumla ya wakazi inakadiriwa kufikia milioni 65, ni kuongezwa kwa ufadhili wa kifedha huku ukosoaji ukizidi kuhusu kasi ndogo ya utekelezaji wa ahadi zilizotolewa awali na Umoja wa Mataifa.

Mkutano huo unatarajiwa kukamilika Alhamisi wiki hii, huku washiriki wakitarajiwa kuafikiana juu ya mpango kazi utakaotumika kwa kipindi cha miaka kumi ijayo.

Wafuatiliaji wanasubiri kuona kama jumuiya ya kimataifa itafanikiwa kukubaliana kuzipa nchi ndogo za visiwa zinazoendelea msaada wa muda mrefu, ikiwa ni pamoja na mpango wa kuzisaidia kulipa madeni yao, na mfumo mpya wa kuzisaidia kifedha.

(afpe)