Papa asema dini isitumiwe kwa malengo ya kisiasa
14 Septemba 2021Papa Francis yuko ziarani nchini Slovakia, ambako ameongoza misa ndefu maarufu kama Liturujia takatifu, ambayo ni ibada inayotumiwa na makanisa ya Kikatoliki ya Mashariki na Orthodox.
Hotuba ya Papa Francis imejikita kwenye utambulisho wa Kikristo, akisema misalaba mara nyingi hutumiwa kijuuju na Wakristo. Akiwahutubia waumini takriban elfu 30, Francis amesema Wakristo wengi wanayo misalaba shingoni mwao, kwenye kuta majumbani mwao, kwenye magari yao na hata mifukoni mwao, lakini hawana uhusiano wa kweli na Yesu.
Soma pia: Papa Francis awahimiza Wakristo kutopoteza tumaini
"Itakuwa na maana gani kama hatujafungua mioyo yetu kwa Yesu aliesulubiwa na kufungua mioyo yetu kwake? Tusiushushe msalaba kuwa tu kitu cha ibada, kuwa ishara tu ya kidini na hadhi ya kijamii," alisema Papa.
Mnamo mwaka 1950 mjini Presov, watawala wa kikomunisti waliwalaazimisha wakotoliki wa kanuni ya ibada ya Mashariki, ambao ni watiifu kwa papa, kujiunga na kanisa la Orthodox, ambapo viongozi kadhaa wa madhehebu hayo waliokataa walifungwa jela.
Nchini Hungary, ambako papa alisimama kwa muda siku ya Jumapili, waziri mkuu Viktor Orban amekuwa akitumia hisia za kidini katika siasa zake za kizalendo na kupinga uhamiaji, akisema kwamba urithi wa kikristo wa Hungary uko hatarini kutoweka.
Baada ya mkutano wake na papa, Orban alisema alimuomba kiongozi huyo kutowaacha wakristo wa Hungary kuangamia.
Papa alisema akiwa Hungary kwamba nchi hiyo inaweza kuhifadhi mizizi yake ya kikristo huku ikifungua milango kwa watu wenye uhitaji.
Soma pia: Papa Francis awaombea wahanga wa hujuma za kundi la IS
Wakati wa Liturujia ya leo Jumanne, papa Francis alionekana tena kuwaonya Wakristu dhidi ya kutumia dini yao katika kile kinachoitwa vita vya utamaduni ambavyo anaamini vinaumiza manufaa ya pamoja. " Ni mara ngapi tunatamani ukristo wa washindi?, alihoji Papa.
Msalaba siyo bendera
Nchini Slovakia, chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Kotlebovci-People's Party Our Slovakia, kinasema kinasimamia nguzo tatu - ambazo ni Ukristo, kitaifa na kijamii, na kimeapa kuzuwia uhamiaji wa wakimbizi ambao wengi ni Waislamu.
"Msalaba siyo bendera ya kupeperusha, lakini chanzo halisi cha njia mpya ya kuishi - njia ya injili na heri. Shahidi anaebeba msalaba moyoni mwake, na siyo tu kifuani, hamtazami yeyote kama adui, lakini kama kaka au dada ambaye kwa ajili yake Yesu alitoa maisha yake", alisema Papa Francis.
Vyama kadhaa vya kisiasa barani Ulaya, vikiwemo vya mrengo mkali wa kulia katika Ulaya Mashariki, hutumia misalaba kwenye bendera zake au kama nembo zake.
Nchini Hungary, mshirika wa serikali ya Orban, cham kidogo cha Christian Democratic People's Party, KDNP, kinatumia msalaba kwenye nembo yake.
Chama cha siasa kali za kizalendo cha mrengo wa kulia, pia hutumia msalaba wa Byzantine wenye mihimili miwili iliyolala sawasawa.
Chanzo: rtre,ap