1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis: Ongezeko la joto ni changamoto kubwa duniani

4 Oktoba 2023

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi na kukosoa hali ya kutozingatiwa kwa kitisho kilichopo kinachofanywa na wanasiasa.

https://p.dw.com/p/4X75D
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa FrancisPicha: Ettore Ferrari/ANSA/picture alliance

Papa Francis amewataka viongozi wa ulimwengu katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira wa COP 28 huko Dubai kupunguza ongezeko la joto duniani kabla hawajachelewa. 

Katika waraka wake mpya wa kitume uliopewa jina ''Laudate Deum'' yaani ''Mungu apewe Sifa'' ambao umechapishwa leo, Papa Francis amesema ongezeko la joto ni moja ya changamoto kubwa zinazoikabilia jumuia ya kimataifa.

Katika muendelezo wa Waraka wa ''Laudato Si'' yaani ''Sifa Ziwe Kwako'' aliouchapisha mwaka 2015 kuhusu mazingira, Papa Francis amesisitiza kuhusu madhara ambayo tayari yapo kwa binadamu na dunia, akisema watu masikini na walio hatarini zaidi duniani ndiyo wanaathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi.

''Kwa sasa hatuwezi kusitisha uharibifu mkubwa ambao tumeusababisha, hatuna muda wa kuzuia madhara makubwa zaidi.''

Wito wa kusitishwa kwa nishati ya visukuku

Kampuni ya nishati ya RWE ya Ujerumani kufunga kiwanda cha nishati ya makaa ya mawe
Kampuni ya nishati ya RWE ya Ujerumani kufunga kiwanda cha nishati ya makaa ya mawePicha: Ina Fassbender/AFP

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki amesema wakati wa kipindi cha mpito kuelekea katika matumizi ya nishati isiyochafua mazingira, kama vile nishati ya upepo na jua, na kuachana na matumizi ya mafuta, haiendelei kwa kasi inayohitajika.

Ametaka mazungumzo ya COP28 yatakayoanza Dubai, Novemba 30 mwaka huu, kuwasilisha mabadiliko ya mwelekeo, kwa viongozi kujizatiti zaidi kuachana na matumizi ya gesi chafu ya kaboni.

Katika waraka wa "Laudato Si," Papa Francis alitoa wito wa "uongofu wa Kiikolojia" na akashutumu uharibifu wa mazingira, ukosefu wa haki wa kijamii na kulinda maslahi ya watumiaji.

Katika waraka wa Laudate Deum, Papa Francis, mwenye umri wa miaka 86 amegusia pia udhaifu wa kisiasa kimataifa na kusema kuwa udhaifu wa taasisi na mashirika ya kimataifa zinakwamisha uwezo wa kuheshimu juhudi zilizochukuliwa na kutatua migogoro.

Mapema asubuhi wakati akifungua Sinodi ya Maaskofu ulimwenguni, Papa Francis amewataka viongozi wa Kikatoliki kuweka pembeni tofauti zao na kufanya kazi kwa ajili ya kulifanya kanisa liwe sehemu ambapo watu wote wanakaribishwa.

Soma pia: Guterres aitaka dunia kuifanya Afrika kuwa nguvu ya nishati jadidifu

Amesema maaskofu wanapaswa kuepukana na mikakati ya kibinadamu, na vita vya kiitikadi au kisiasa.

Wahafidhina wanaomkosoa Papa wamezidi kupaza sauti hata kabla ya kuanza kwa Sinodi hiyo ambayo itajadili mada mbalimbali ikiwemo ushiriki na nafasi ya wanawake ndani ya kanisa, kukubalika kwa Wakatoliki wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambazo zinawapata zaidi masikini.

Mwadhama Raymond Kardinali Burke, askofu wa Marekani mwenye makaazi yake mjini Roma, ambaye ni mmoja wa wakosoaji wakubwa wa Papa Francis, ameonya kuhusu sumu ya migawanyiko inayoweza kujitokeza katika Sinodi, na kusema kuwa wanapaswa kudhihirisha imani yao hadharani.

Amebainisha kuwa katika hilo, maaskofu wana wajibu wa kuwathibitishia ndugu zao, maaskofu na kwamba makardinali wa leo wanahitaji ujasiri mkubwa wa kukabiliana na makosa makubwa yanayotoka ndani ya kanisa lenyewe.