1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi wakabiliana na waandamanaji Paris kuhusu pasi ya afya

1 Agosti 2021

Maelfu ya maafisa wa polisi wametawanywa kote mjini Paris kukabiliana na waandamanaji wanaopinga kuanzishwa pasi maalumu ya afya kwa wale waliochanjwa dhidi ya virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3yNWd
Frankreich Protest gegen Corona-Regeln
Picha: Adrienne Surprenant/AP Photo/picture alliance

Zaidi ya polisi 3,000 na maafisa wa usalama wameuzunguka mji mkuu wa Ufaransa Paris Jumamosi wakati maelfu ya waandamanaji wakiwa wamekasirishwa na mpango wa serikali wa kuanzisha pasi maalumu kwa waliopigwa chanjo dhidi ya virusi vya corona.

Nchini kote, watu wapatao 204,000 wameshiriki maandamano hayo, kulingana na Wizara ya Mambo ya Ndani. Idadi hiyo ya watu imeongezeka ikilinganishwa na ile ya wikiendi iliyopita.

Soma zaidi: EU: Yapendekeza pasi maalum ya chanjo ya virusi vya corona

Katika jiji la Paris, polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji katika mikusanyiko minne tofauti mjini humo.

Polisi hao walikuwa wanajaribu kuwazuia waandamanaji kuingia katika barabara maarufu ya Champs-Elysee, ambayo ilitawaliwa na maandamano ya "vizibao vya manjano" yaliyokuwa na vurugu mnamo mwaka 2018.

Msemaji wa polisi amesema maafisa watatu wa polisi wamejeruhiwa na waandamanaji wakati wa makabiliano hayo ya siku nzima.

Frankreich Protest gegen Corona-Regeln
Waandamanaji Ufaransa wanaopinga sheria za kujikinga na virusi vya coronaPicha: Michel Euler/AP/dpa/picture alliance

Wafaransa wanaandamana kupinga nini?

Kuanzia Agosti 9, pasi mpya za afya zitahitajika kwa raia kuweza kusafiri na kuingia kwenye maeneo ya biashara, kama vile migahawa, vinyozi, pamoja na kupanda kwenye treni au kushiriki kwenye maonyesho tofauti, pendekezo hilo bado linasubiri idhini ya Baraza la Katiba. Aidha upigaji wa chanjo dhidi ya virusi vya corona itakuwa lazima kwa baadhi ya wafanyakazi.

Maandamano hayo yamekuwa yakiendelea kwa Jumamosi ya tatu mfululizo. Na hayafanyiki tu mjini Paris, lakini pia kwenye miji mingine ipatayo 100 nchini kote, ikiwa ni pamoja na Montpellier, Bordeaux, Marseille na Nice. Afisa wa wizara ya mambo ya ndani amesema zaidi ya watu 200,000 wameandamana kote Ufaransa.

Nani anaeandamana Ufaransa?

Utafiti wa maoni ya raia unaonyesha kwamba idadi kubwa ya watu Ufaransa inaunga mkono mpango huo wa pasi maalumu ya afya, lakini baadhi wanaikataa hatua hiyo, na kuamua kumiminika barabarani kuipinga serikali kwa hasira.

Waziri wa mambo ya ndani Gerald Darmanin amefafanua zaidi suala hilo.

"Unapoona watu milioni 4 waliokwenda kupata chanjo baada ya hotuba ya rais, basi unakubali kwamba waandamanaji hawapo wengi," ameliambia gazeti la Le Parisien.

Frankreich Protest gegen Corona-Regeln in Paris
Waandamanaji Ufaransa wanaopinga sheria za kujikinga na virusi vya coronaPicha: Sarah Meyssonnier/REUTERS

Je kila mtu anapinga mpango huo wa kuwa na pasi maalumu ya afya?

Wananchi wengine wamekubali kupigwa chanjo, ili waweze kuishi maisha yao kwa uhuru katika kipindi hiki cha mapumziko Ufaransa cha mwezi wa Agosti.

Serikali ya shirikisho na za majimbo kote nchini zimeandaa vituo tofauti ambayo watu wanaweza kwenda kupigwa chanjo kiurahisi, ikiwa ni pamoja na karibu na fukwe za bahari ambako watu wengi wanakwenda kwa mapumziko katika kipindi hiki cha msimu wa joto.

Soma zaidi: Macron: Wanawake wameathirika zaidi na COVID-19

Maambukizi ya virusi vya corona yaliyotokana na aina mpya iitwayo Delta yameongezeka nchini Ufaransa. Siku ya Ijumaa pekee, kumeripotiwa maambukizi mapya ya watu 24,000.

Kulingana na utafiti mpya uliofanywa na Wizara ya Jamii na Afya, watu ambao hawakupata bado chanjo ni asilimia 85 ya wanaougua ugonjwa wa COVID-19 hospitalini - ikiwa ni pamoja na wale waliolazwa kwenye vyumba vya kutunza wagonjwa mahatuti.

Watu wapatao 112,000 wamefariki dunia Ufaransa kutokana na virusi vya corona tangu janga hilo kuanza mwaka jana. Na hadi hivi sasa asilimia 52 ya watu wa Ufaransa tayari wameshachanjwa.