Israel na kundi la Hamas warefusha usitishaji mapigano
28 Novemba 2023Tangazo la kurefushwa mkataba wa kusitisha mapigano kati ya pande hizo hasimu linazingatiwa kuwa ahueni nyingine kwenye mzozo huo wa Mashariki ya Kati ulioingia wiki ya saba.
Kulingana na maafisa wa Qatar, taifa lililojitwika dhima ya kuwa mpatanishi wa mzozo unaoendelea, makubaliano hayo mapya yatakuwa ya siku mbili na kuna matumaini yatajumuisha kuachiwa mateka zaidi wa Israel waliokamatwa na kundi la Hamas.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Qatar ni miongoni mwa maafisa walioeleza habari hizo kupitia mtandao wa kijamii wa X zamani ukifahamika kama Twitter.
Katika usitishaji wa kwanza wa siku nne uliomalizika jana, kila siku kundi la Hamas lilikuwa likiwaachia mateka kadhaa wa Israel.
Hapo kabla Israel ilikwishasema itakuwa tayari kurefusha makubaliano ya kusitisha hujuma zake kwa kila siku kwa mabadilishano ya mateka 10.
Matumaini ni makubwa wakati Israel inasubiri serikali kutoa idhini
Hata hivyo, Israel bado inasubiri idhini ya serikali nzima kabla ya makubaliano yaliyotangazwa jana kuanza kufanya kazi. Shirika la Habari la Reuters limeripoti kwamba Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ameiomba serikali yake ikubali kurefusha mkataba wa kusitisha operesheni zake huko Ukanda wa Gaza kwa ahadi ya mateka zaidi kuachiwa huru na Hamas.
Maafisa wa Qatar ambao wanashirikiana na Marekani kuratibu mashauriano kati ya Israel na kundi la Hamas wamesema wana imani kubwa kwamba usitishaji mapigano kwa siku mbili zaidi utaidhinishwa nchini Israel bila ya mashaka.
Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu amesema rais wa Marekani Joe Biden amesaidia sana kufanikisha makubaliano hayo ya sasa yatakayowezesha kuachiwa mateka zaidi bila upande wa Israel kutimiza matakwa mengi ya kundi la Hamas.
Hata hivyo, amesisitiza kwamba malengo ya Israel kwenye vita vyake dhidi ya Hamas hayajabadilika.
"Kuhusiana na suala la mateka, tunaendelea kutekeleza tulichokubaliana na pia tunaendelea na lengo letu kuu tulilolitaja - kuhakikisha mateka wetu wanarejea nyumbani, kulitokomeza kabisa kundi la Hamas, na bila shaka vilevile kuhakikisha kwamba kitisho hiki hakitajirudia tena ndani ya Gaza, na hakutakuwa na utawala wowote unaopigia pambaja ugaidi, kufundisha ugaidi na kuugharamia". amesema Netanyahu.
Mateka zaidi waachiwa huru ikiwemo vijana wawili wa Kijerumani
Tangu awamu ya kwanza ya usitishaji mapigano ilipoanza Ijumaa iliyopita, jumla ya mateka 69 wameachiwa huru na kundi la Hamas kwa mabadilishano ya kiasi wafunga 150 wa Kipalestina na msaada mkubwa wa kiutu kuruhusiwa kuingia Ukanda wa Gaza.
Inaaminika zaidi ya mateka 200 walichukuliwa na kundi la Hamas. Hapo jana wengine zaidi waliachiwa huru ikiwemo vijana wawili raia wa Ujerumani.
Wakati hayo yakijiri upande wa Palestina umerejelea rai yake ya kuitaka Jumuiya ya Kimataifa itafute njia za kukomesha mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.
Mwanadiplomasia mkuu wa serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina Riad al-Maliki ametoa mwito huo wakati wa mkutano unaowakutanisha mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya na mataifa ya kiarabu huko Barcelona.
Al Maliki amesema ni lazima itafutwe njia ya kuongeza shinikizo dhidi ya Israel ili isitishe kile alichokitaja kuwa "mauaji ya raia wasio na hatia". Amesema pindi muda wa kusitisha mapigano utakapomaliziika na Israel ikaanza tena mashambulizi yake, vifo zaidi vitatokea.
Hadi sasa mamlaka za Ukanda wa Gaza zinasema watu wapatao 14,000 wameuwawa tangu Israel ilipoanza kufanya mashambulizi yake ya kulipiza kisasi kwa shambulizi kubwa lililofanywa na kundi la Hamas ndani ya ardhi yake.
Shambulizi hilo la Oktoba 7 liliwauwa watu 1,200. Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine kadhaa ya magharibi yameliorodhesha kundi la Hamasi kuwa la kigaidi.
Blinken kurejea tena Mashariki ya Kati kushughulikia mzozo
Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Antony Blinken atafanya ziara nyingine Mashariki ya Kati baadae wiki hii ikiwa ni ya tatu tangu kuzuka mapigano Ukanda wa Gaza.
Hayo yameelezwa na ofisi yake jana Jumatatu. Ziara hiyo itamkutanisha na waziri mkuu wa Israel mjini Tel Aviv Benjamin Netanyahu na rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mamhoud Abbas mjini Ramallah.
Ananuia kupigia debe umuhimu wa kuendelea kuingizwa msaada wa kiutu kwenye Ukanda wa Gaza, kufanikisha kukombolewa mateka wote na kuimarisha ulinzi wa raia huko Gaza.
Vyanzo: reuters/ap