Moldova yapiga kura kumchagua rais, kuamua hatma kujiunga EU
20 Oktoba 2024Wapiga kura nchini Moldova wanapiga kura kumchagua Rais wao na kuamua hatma ya Jamhuri hiyo kuhusu kujiunga na Umoja wa Ulaya. Msemaji wa tume ya uchaguzi nchini humo Angelica Caraman amesema tayari zoezi la kupiga kura limeanza bila matatizo na maelfu ya watu wameshapiga kura.
Katika uchaguzi huo wenye wagombea 11, Rais Maia Sandu 52, anayeunga mkono Umoja wa Ulaya anatetea kiti chake. Sandu anayepewa nafasi kubwa ya kushinda anaituhumu Urusi kwa kujaribu kuiteteresha Moldova kwa kusambaza habari za uongo na kuchochea maandamano dhidi ya serikali.
Soma zaidi: Urusi yatuhumiwa kuingilia uchaguzi wa serikali za mitaa Moldova
Raia nchini humo wanapiga pia kura ya maoni kuhusu kujiunga na Umoja wa Ulaya. Matokeo ya kura hiyo yataamua iwapo nchi hiyo itajiunga na Umoja wa Ulaya au itaendeleza ushirikiano wa kiuchumi na Urusi. Moldova, iliyo kati ya Romania na Ukraine nayo inawania kujiunga na umoja huo kama ilivyo Ukraine.