Rais Macron awasili Lebanon kuonyesha uungwaji mkono
17 Januari 2025Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliwasili Beirut siku ya Ijumaa katika ziara inayolenga kuunga mkono uongozi mpya nchini Lebanon.
Macron alikutana na waziri mkuu wa muda Najib Mikati alipowasili katika uwanja wa ndege wa Beirut na anatazamiwa kukutana na Rais wa Lebanon Joseph Aoun na waziri mkuu mteule Nawaf Salam.
"Nimefurahi sana kuwa hapa, na nilitaka kutoa shukrani zangu kwa Waziri Mkuu kwa kuiongoza nchi kwa muda wote kwa maslahi ya kila mtu na ya Lebanon, na haswa katika miezi hii michache iliyopita, ambayo imekuwa migumu sana na hasa kutokana na vita," alisema Rais Macron.
Mikati amesema wamezungumza na Macron juu ya hali ya sasa na umuhimu wa kuendelea kusaidia Lebanon katika ngazi zote, kiuchumi na katika ujenzi mpya.Rais wa Lebanon amteua jaji wa ICJ kuwa waziri mkuu
Amesema Macron yuko tayari kuiunga mkono Lebanon na anakusudia kujadiliana na Benki ya Dunia jinsi ya kusaidia kulijenga upya eneo la kusini mwa nchi hiyo lililoharibiwa.
Macron pia anatarajiwa kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ambaye pia yuko Lebanon.