Rais wa Lebanon amteua jaji wa ICJ kuwa waziri mkuu
14 Januari 2025Kufuatia mashauriano na wabunge ili kuunda serikali itakayoondoa taifa hilo lililokubwa na vita katika mgogoro wa muda mrefu wa kiuchumi.
Taarifa kutoka kwa ofisi ya rais imesema kwamba wabunge wengi wa Lebanon walimuidhinisha Salam aliyeteuliwa jana na Rais Aoun, kuunda serikali.
Soma pia: Lebanon: Rais mpya aibua matumaini ya utulivu Mashariki ya Kati
Kulingana na hesabu ya vyombo vya habari vya Lebanon, wabunge 84 walimuunga mkono Salam huku tisa wakimpendekeza waziri mkuu wa muda, Najib Mikati, kusalia katika nafasi hiyo na 35 wakikataa kuunga mkono mgombea yeyote.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu jioni, Rais Aoun alisema anatumai hatua ya kuunda serikali itakuwa "shwari na haraka iwezekanavyo".
Lakini Firas Hamdan, mmoja wa takribani wabunge kumi na wawili waliochaguliwa baada ya maandamano makubwa dhidi ya serikali mnamo 2019, amesema uteuzi wa Salam ulikuwa "mpango wa kisiasa wa Lebanon" usio na mwingiliano wowote wa kigeni.
Wafuasi wa waziri mkuu wa muda mrefu, Najib Mikati, wanamwona jaji na balozi huyo wa zamani kama mtu asiye na upendeleo anayeweza kufanya mageuzi yanayohitajika sana.
Lakini wakosoaji wa Mikati wanamuona kama nembo ya mfumo wa siasa za kibaraka ambao pia ulijumuisha Hezbollah na kuiongoza nchi kuelekea kuporomoka kifedha.
Changamoto katika kuunda serikali
Waziri mkuu mpya atakabiliwa na changamoto kubwa, ikiwa ni pamoja na kutekeleza mageuzi ya kuridhisha wafadhili wa kimataifa ili kuiondoa nchi hiyo katika mdororo mbaya zaidi wa kifedha katika historia yake.
Pia atakabiliwa na jukumu kubwa la kujenga upya maeneo ya Lebanon yaliyoharibiwa katika vita vya Israel na Hezbollah, pamoja na kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano.
Soma pia: Israel imefanya mashambulio katika maeneo mbali mbali ya Lebanon
Mbunge Georges Adwan wa Lebanese Forces, chama kikuu cha Kikristo, alisema baada ya kumuidhinisha Salam kwamba ni wakati wa Hezbollah kuzingatia kujiunga na kisiasa akihoji kwamba "enzi ya silaha imekwisha."
Raia wa Lebanon wameonyesha kuridhishwa na uidhinishwaji huu kama anavyoeleza Samar Haidar:
"Waziri Mkuu Nawaf, ni Jaji wa mahakama, ni mjuzi sana, na ni mzuri sana, anaweza kuendesha nchi, Mungu akipenda, na anaweza kuunda serikali, Mungu akipenda, atakuwa na matokeo chanya.
"Lolote atakaloahidi atalitimiza - na chini ya serikali hii, nchi itasonga mbele na mambo yatatulia lakini kwa kweli ni mwema, na Mungu akipenda ataiendesha nchi vizuri."
Mgawanyiko na ushindani
Chanzo karibu na kundi la Hezbollahkiliiambia shirika la habari la AFP kabla ya mashauriano ya Jumatatu kwamba kundi hilo na mshirika wake vuguvugu la Amal walimuunga mkono Mikati.
Kwa mujibu wa katiba ya Lebanon, rais humteua waziri mkuu baada ya mazungumzo na vyama vyote vya siasa na wabunge huru bungeni. Kwa makubaliano, huchagua mgombea aliye na kura nyingi wakati wa mashauriano haya.
Hata hivyo, kuteuliwa kwa waziri mkuu hakuhakikishi kuwa serikali mpya itaundwa mara moja. Mchakato huo hapo awali umechukua wiki au hata miezi kutokana na mgawanyiko mkubwa wa kisiasa na ushindani.