Rais Ruto atangaza mikakati ya kukabiliana na mafuriko
25 Novemba 2023Rais wa Kenya William Ruto amesema hii leo kuwa nchi hiyo inapanga mikakati ya kukabiliana na maafa yaliyotokana na mafuriko ambayo yamesababisha vifo vya watu 70 na kupelekea makumi ya maelfu ya wengine kuyahama makazi yao na kusema hiyo ni "hali ya dharura".
Ruto ameyasema hayo baada ya kufanya mazungumzo na timu mbalimbali za kukabiliana na maafa na kusisitiza kuwa baraza la mawaziri litakutana siku ya Jumatatu kujadili mapendekezo ya namna ya kudhibiti mafuriko hayo.
Aidha Ruto amesema serikali imetoa shilingi bilioni 2.4 (karibu dola milioni 16) ili kutoa chakula kwa raia waliohamishwa na mafuriko.
Nchi za mashariki na Pembe ya Afrika kama Kenya, Somalia na Ethiopia zinakabiliwa na mvua kubwa za El Nino ambazo zinatarajiwa kudumu eneo hilo hadi angalau mwezi Aprili mwakani.