Afrika Kusini: Rais atangaza ANC itaunda serikali ya umoja
7 Juni 2024Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametangaza rasmi kwamba chama chake cha African National Congress (ANC) kitaunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Katika uchaguzi mkuu wa wiki jana ANC ilipata ushindi kwa zaidi ya asilimia 40 ya kura na viti 158 katika Bunge la Afrika Kusini, lakini hata hivyo kwa mara ya kwanza katika historia yao, chama hicho tawala kilipungukiwa na wingi wa kutosha kuweza kutawala peke yake.
Mkutano wa ANC na vyama vyote vya upinzani
Baada ya majadiliano ya saa kumi na wanachama wakuu wa chama tawala cha ANC, Rais Cyril Ramaphosa amekiri kwamba ANC sasa inahitaji washirika ili kuunda serikali.
Soma pia: ANC yashindwa kupata wingi wa kura bungeni
Ramaphosa amesema, "mazungumzo kama hayo ya kitaifa yataimarisha kazi kubwa ya kujenga upya uwiano wa kijamii katika jamii iliyoshuhudia kampeni ya uchaguzi yenye migawanyiko."
Akihimiza kwamba pande zote lazima zijitolee katika ujenzi wa taifa kwa pamoja, amesisitiza umuhimu wa kuheshimu katiba ya Jamhuri ya Afrika Kusini na utawala wa sheria, haki ya kijamii na usawa, utu wa binadamu, kutokuwa na ubaguzi wa rangi wala ubaguzi wa kijinsia.
"ANC inabainisha kuwa tuna tofauti za kiitikadi na kisiasa na vyama kadhaa katika mazingira yetu ya kisiasa. Hata hivyo, hatutazuia uwezekano wa kufanya kazi na chama chochote ili mradi ni kwa maslahi ya umma na inazingatia kanuni nilizozieleza," amesema.
Kauli za vyama vya kisiasa
Tayari ANC imefanya mazungumzo na vyama vitano vya siasa, ambavyo ni; chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto, EFF, chama cha Zulu cha Inkatha Freedom Party (IFP), chama cha mrengo wa kulia cha Democratic Alliance (DA), National Freedom Party (NFP) na chama cha kupinga wahamiaji Patriotic Alliance (PA).
Soma pia: ANC yazidi kupoteza uungaji mkono - Utafiti
Mapema hii leo chama cha Inkatha Freedom Party (IFP) kimetangaza kwamba hakipingi wazo la kuunda serikali ya umoja wa kimataifa. Kupitia taarifa rasmi, IFP imesema, "utata uko katika maelezo, ambayo yatakuwa wazi zaidi katika siku zijazo."
Chama cha Zuma, ambacho kimepata asilimia 14.6 ya kura zote, kimekataa matokeo ya uchaguzi na kutishia kususia bunge. Pia chama hicho cha Umkotho Wesizwe kimesema hakitaunga mkono serikali inayoongozwa na ANC ikiwa Ramaphosa ataendelea kushikilia usukani.
Tayari chama cha Democratic Alliance (DA) kimesema hakitajiunga na serikali ambayo itawashirikisha pia Umkotho Wesizwe na EFF.