Buriani Rais wa Namibia Hage Geingob
4 Februari 2024Makamu wa Rais wa Namibia Nangolo Mbumba alitangaza kifo cha rais Hage Geingob na kusema kuwa kiongozi huyo aliaga dunia majira ya saa sita usiku.
Ofisi ya Rais wa Namibia imesema Kiongozi huyo wa Nambia Hage Geingob aliaga dunia huku mkewe, Monica Geingob, na watoto wao wakiwa kando yake.
Salamu za rambirambi kutoka kwa viongozi mbalimbali wa Afrika zilimiminika siku ya Jumapili 04.02.2024 kutokana na kifo cha Rais wa Namibia Hage Geingob.
Salamu za rambirambi za viongozi wa Afrika
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, amesema: "Afrika Kusini inaungana na watu wa Namibia kuomboleza kifo cha kiongozi, mzalendo na rafiki wa Afrika Kusini.
Ramaphosa amesema Rais Geingob alikuwa mwanajeshi mkongwe wa ukombozi wa Namibia kutoka kwa wakoloni na wabaguzi wa rangi.
Rais William Ruto wa Kenya alirejea sifa hizo kwa marehemu Rais wa Namibia na kuongeza kuwa Geingob aliamini katika Afrika iliyoungana na pia alikuza mwonekano wa bara la Afrika katika nyanja ya kimataifa.
Soma pia:Rais wa Namibia ataka raia weusi wamiliki ardhi zaidi
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameandika kwenye ukurasa wake wa X akisema "Nimehuzunishwa sana na kifo cha Rais wa Namibia Mheshimiwa Hage Geingob ndugu mpendwa, mwanajumuiya wa Afrika na rafiki mkubwa wa Tanzania."
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amechapisha ujumbe kwenye mtandao wa X, akisema "uongozi na uimara wa Geingob vitakumbukwa."
Hage Gottfried Geingob aliingia madarakani mwaka 2015, mpaka kifo chake alikuwa ni rais wa tatu wa Namibia na alikuwa akitumikia muhula wake wa pili uliokuwa wa mwisho.
Awali alikuwa Waziri Mkuu wa Namibia mara baada ya nchi hiyo kupata uhuru wake ambapo alihudumu kwenye wadhfa huo kwa muda mrefu.
Alikuwa mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi na kabla ya kugeuka na kuwa mwanasiasa.
Makamu warais wa Namibia Angolo Mbumba, ambaye anakaimu nafasi ya Rais, ametoa wito wa utulivu, akisema Baraza la Mawaziri litakutanamara moja kutekeleza mipango muhimu ya serikali na kwamba taarifa zaidi zitatolewa.