1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Rais wa Ukraine azungumza na mwenzake wa China

26 Aprili 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amefanya mazungumzo yenye manufaa kwa njia ya simu na Rais wa China Xi Jinping.

https://p.dw.com/p/4Qaul
Bildkombo Selenskyj und Xi Jinping
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy(Kushoto) amefanya mazungumzo na mwenzake wa China Xi Jinping.Picha: Ukrainian Presidentia/IMAGO/MONCLOA PALACE/REUTERS

Rais Zelensky ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kwamba mazungumzo hayo yaliyofanyika Jumatano na kudumu kwa takribani saa moja, yalikuwa yenye manufaa. Amesema anaamini kuwa mazungumzo hayo pamoja na uteuzi wa balozi wa Ukraine nchini China, yatatoa msukumo mkubwa kwa maendeleo ya uhusiano wa nchi hizo mbili.

Soma pia:Brazil yapinga ukosoaji wa Marekani, yatetea mahusiano na Urusi 

Yu Jun, Naibu Mkurugenzi wa idara inayoshughulikia masuala ya Ulaya na Asia katika Wizara ya Mambo ya Nje ya China, amesema Ukraine ndiyo ilianzisha juhudi za kufanyika kwa mazungumzo hayo. Yu amesema Rais Xi amemwambia Zelensky kuwa serikali yake itampeleka mjumbe wa amani Ukraine na kwenye nchi nyingine, baada ya China kusema inataka kuwa mpatanishi katika kusuluhisha vita kati ya Urusi na Ukraine.

''Rais Xi amezungumza kwa njia ya simu na Rais Zelensky kama alivyoomba. China itapeleka wawakilishi maalum wa serikali kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kina na pande zote ili kupata suluhisho la kisiasa la mzozo huo,'' alifafanua Yu.

Ufaransa inaunga mkono juhudi za upatanishi za China

China France Präsident Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Ng Han Guan/AP Photo/picture alliance

Muda mfupi baada ya kufanyika mazungumzo kati ya Zelensky na Xi, Ufaransa imesema inaunga mkono juhudi za upatanishi za China katika kuumaliza mzozo huo. Ofisi ya Rais Emmanuel Macron imeeleza kuwa Ufaransa inahimiza mazungumzo ambayo yatachangia kupatikana kwa suluhisho unaoendana na maslahi ya kimsingi ya Ukraine.

Huku hayo yakijiri, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Dmytro Kuleba ameishutumu Jumuia ya Kujihami ya NATO kwa kutokuwa na "utashi wa kisiasa" kuiruhusu nchi huyo kujiunga na muungano huo wa kijeshi. Katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha Marekani, CNN Kuleba amesema kila kitu kinawezekana iwapo kuna "utashi wa kisiasa."

Kuleba amewatolea wito wanachama wa NATO kuacha visingizio na kuanza mchakato.

Wakati huo huo, Zelensky ameonya kuwa Urusi inatumia vinu vya nishati ya nyuklia kuulaghai na kuusaliti ulimwengu. Matamshi hayo ameyatoa leo wakati wa kumbukumbu ya miaka 37 ya maafa ya nyuklia katika kinu cha nyuklia cha Chernobyl.

Soma pia:Mkuu wa NATO asema Ukraine itajiunga na jumuiya hiyo siku moja 

Zelensky ameandika katika mtandao wa kijamii wa Telegram kuwa majeraha ya Chernobyl bado hayajapona, na uvamizi wa mwaka jana wa Urusi uliuweka tena ulimwengu katika hatari. Rais huyo wa Ukraine amesema wanapaswa kufanya kila linalowezekana ili kulizuia taifa hilo la kigaidi kutumia vinu vya nishati ya nyuklia kuisaliti Ukraine na dunia nzima.

Ama kwa upande mwingine, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema wanajeshi 40 wa Urusi waliokuwa wanashikiliwa mateka nchini Ukraine, leo wamerejea nyumbani baada ya kufanyika mazungumzo. Wote walioachiliwa huru wanapatiwa matibabu na msaada wa kisaikolojia.

(DPA, AP, AFP, Reuters)