1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiUjerumani

Rungu la Mahakama latikisa sehemu ya bajeti ya Ujerumani

22 Novemba 2023

Serikali ya mseto nchini Ujerumani imetumbukia kwenye kizaazaa kinachotishia uthabiti wake, baada ya uamuzi wa Mahakama ya Shirikisho la Ujerumani kuizuia serikali kuchukua mkopo mkubwa kufadhili miradi ya kimkakati.

https://p.dw.com/p/4ZKcl
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: John Thys/AFP/Getty Images

Hali hiyo inafuatia uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Shirikisho la Ujerumani wiki iliyopita wa kuizuia serikali mjini Berlin kuchukua mkopo mkubwa wa kufadhili miradi ya kimkakati katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha.

Uamuzi huo umeleta hamkani miongonini mwa vyama washirika vya SPD, kile cha walinzi wa mazingira, Die Grüne na FDP, kila upande usijue cha kufanya. 

Mapema wiki hii Waziri wa fedha wa Ujerumani Christian Lindner alitangazakuzuia utekelezaji wa bajeti ijayo ya serikali kuu mjini Berlin ili kutekeleza uamuzi mahakama ya shirikisho uliosema sehemu kubwa ya bajeti hiyo inakwenda kinyume na katiba.

Uamuzi huo wa mnamo Novemba 15 unatafsiriwa na wengi kuwa balaa kubwa kwa serikali ya mseto ya vyama vitatu inayoongozwa na kansela Olaf Scholz. Kwa sababu unaizuia serikali kupata fedha kwa njia ya mkopo ambazo zingetumika kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo.

Soma pia:Dalili zaonesha uchumi wa Ujerumani utaboreka 2024

Mtikiso wote huo umetokana na mpango wa serikali ya Kansela Scholz wa kutaka kubadili matumizi ya mkopo wa kiasi euro bilioni 60 uliotengwa kushughulikia janga la virusi la Corona lililozuka mnamo mwaka 2020.

Baada ya janga hilo kupungua makali, serikali ilitaka kutumia fedha hizo kwa ajili ya miradi ya maendeleo hususani ya kushughulikia kadhia ya mabadiliko ya tabianchi.

Miongoni mwa mipango hiyo ni kuzifanyia ukarabati nyumba nyingi nchini Ujerumani kwa kuziwekea miundombinu ya nishati isiyochafua mazingira pamoja na kuipiga jeki miradi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme.

Hata hivyo upande wa upinzani unaoongozwa na wahafidhina wa vyama ndugu vya CDU na CSU ulifungua shauri mahakamani kupinga mpango huo na mahakama imetoa uamuzi ulowapa ushindi.

Mahakama: Fedha za dharura hazipangiwi matumizi mengine

Mahakama imesema itakuwa ni kinyume na katiba kwa serikali kubadili matumizi ya mkopo uliopangwa kwa ajili ya kushughulikia jambo la dharura.

Imesema chini ya sheria za Ujerumani fedha za dharura haziwezi kupangiwa matumizi ya miradi mingine tena ile ya muda mrefu.

Kadhalika, mahakama imeikumbusha serikali kuwa inawajibika kuanza tena kutekeleza ibara ya katiba inayoweka ukomo wa kiwango cha mikopo. Utekelezaji wa ibara hiyo ulisimama kwa muda wakati wa janga la virusi vya corona.

Waziri wa Uchumi Robert Habeck akiteta na Kansela Olaf Scholz
Waziri wa Uchumi Robert Habeck akiteta na Kansela Olaf ScholzPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Chini ya kile kinachofahamika kama"ukomo wa madeni” serikali ya Ujerumani inazuiwa kikatiba kuchukua mikopo mipya inayopindukia asilimia 0.35 ya pato ghafi la taifa.

Kwa jumla uamuzi huo wa mahakama unamaanisha kwamba serikali ya kansela Scholz inalazimika kuifumua na kuipanga upya bajeti yake ya mwaka ujao. Vilevile inafaa itafute suluhu ya njia zipi itatumia kupata fedha za kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele vyake hali inayotishia kuzusha mivutano.

Soma pia:Scholz: Ujerumani kukuza mahusiano ya kibiashara na Nigeria

Chama cha kansela Scholz cha SPD tayari kimeashiria kutaka kupandisha kiwango cha kodi ili kufidia nakisi itakayojitokeza. Ijapokuwa wanasiasa wa chama hicho wanatumia lugha ya tahadhari kwa sababu SPD hujitapa kuwa chama kinacholinda maslahi ya watu wa kipato kidogo na kile cha kati kwa kujiepusha kuwaongezea mzigo wa kodi.

Hata hivyo ziko sauti zinazoonesha kupinga mawaz hayo. Kiongozi wa kundi la wabunge wa SPD Rolf Mützenich ameirai serikali itafute njia nyingine isiyo ya kuongeza kodi.

Nyongeza ya kodi kuwa mbadala?

Pendekezo la nyongeza ya kodi halikubaliki pia kwa chama mshirika serikalini cha FPD. Chama hicho kinachoendelea biashara hakitaki mzigo mkubwa wa kodi na badala yake kinapendekeza serikali ipunguze matumizi katika kile kinachofahamika kama "hatua za kufunga mkwiji”

Msimamo huo umeelezwa waziwazi na Waziri wa fedha wa Ujerumani kutoka FDP Bw. Christian Lindner.

Je, uhamiaji ni tishio kwa Ujerumani?

Hata hivyo tatizo ni kwamba pendekezo hilo la kupunguza matumizi litawakasirisha sana washirika wengine wa serikali wa chama cha kijani, Die Grüne.

Soma pia:Ujerumani kuwa nchi ya pekee barani Ulaya kuingia kwenye mdororo wa uchumi 2023

Hatua yoyote ya kubana matumizi itamaanisha miradi yote ya uwekezaji ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi itakosa fedha. Hilo haliwezi kupekelewa vyema na chama kinachopigania ulinzi wa mazingira na ambacho ajenda yake kwa wapigakura ni hiyo.

Kwa jumla yote hayo yanaifanya serikali ya mseto ya Ujerumani kuwa njiapanda. Kansela Scholz amejitahidi kuonesha sura ya ukakamavu wiki hii akiliambia bunge kwamba serikali anayoiongoza itatafuta majibu sahihi na itavuka mtihani inaopitia.

Lakini kwa wafuatiliaji wa siasa za Ujerumani, kingóra cha tahadhari tayari kinalia mjini Berlin na kitisho cha "kugawana mbao” ndani ya jahazi la kansela Scholz kinanukia.