1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sarkozy ahukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela

30 Septemba 2021

Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na korti ya Paris Alhamisi baada ya kukutwa na hatia katika kesi ya ufadhili wa kampeni yake ya Urais ya mwaka 2012. 

https://p.dw.com/p/415e7
Frankreich | Prozess Ex-Präsident Sarkozy
Picha: Stephane De Sakutin/AFP/Getty Images

Sarkozy aliyeiongoza Ufaransa kati ya mwaka 2007 hadi 2012, licha ya hukumu hiyo huenda akaepuka kwenda jela. Jaji aliyetoa hukumu hiyo amesema Sarkozy anaweza kutumikia kifungo cha nyumbani japo atavishwa kifaa maalum cha kieletroniki cha kumfwatilia.

Rais huyo wa zamani wa Ufaransa, kupitia wakili wake Thierry Herzog amesema atakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

" Rais Sarkozy ambae tumezungumza kwa njia ya simu, kaniomba nikate rufaa. Nitafanya hivyo mara moja, na hivyo uamuzi huu hautatekelezwa."

Hata hivyo, Sarkozy amekuwa akikanusha kuhusika na makosa yaliyokuwa yakimkabili katika kesi hiyo maarufu kama "Bigmalion" iliyoendeshwa mwezi Mei na Juni mwaka huu. Leo hii amekutwa na hatia ya ufadhili haramu katika kampeni yake.

Sarkozy, anatuhumiwa kutumia karibu mara mbili ya kiwango cha fedha kinachoruhusiwa kisheria ikiwa ni kiasi cha Euro milioni 22 na nusu katika kampeni yake ya kugombea muhula wa pili wa urais katika uchaguzi alioshindwa na Francois Hollande.

Awali, waendesha mashtaka walipendekeza Sarkozy ahukumiwe kifungo cha mwaka mmoja ambacho miezi sita angelitakiwa kukaa gerezani na miezi 6 mingine atumikie kifungo cha nje, na pia kulipa faini ya euro 3,750 sawa na dola za kimarekani 4,354.

Hukumu hii inatolewa wakati ambapo Sarkozy mwenye umri wa miaka 66 alikata rufaa baada ya kukutwa na hatia mwezi Machi katika kesi nyengine ya ufisadi ambapo anadaiwa kumuhonga jaji ili apate taarifa za siri kuhusu kesi ya uchunguzi dhidi yake.

Rais huyo wa zamani alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela katika kesi hiyo, miwili ambayo ilifutwa, lakini bado hajatumikia kifungo gerezani.

Frankreich | Wahlkampfkosten-Prozess gegen Ex-Präsident Nicolas Sarkozy
Thierry Herzog wakili anayemtetea Sarkozy (katikati)Picha: Alain Jocard/AFP/Getty Images

Na katika kesi hii ya ufadhili wa kampeni, waendesha mashtaka walihitimisha kwa kusema kuwa Sarkozy alifahamu vyema kuwa matumizi yake ya pesa yalizidi kiwango kinachoruhusiwa kisheria na hivyo kupuuza hata ushauri wa mahasibu wake waliomuonya juu ya kufanya hivyo, huku akiendelea kuchupa mipaka kwa kuandaa mikutano mingi na mikubwa wakati wa kampeni yake.

Wakati wa kusikilizwa kwake, Sarkozy alijitetea kuwa pesa za ziada hazikutumiwa katika kampeni yake bali kuwatajirisha baadhi ya watu na kusema kuwa kesi hiyo ni ulaghai mtupu. Alisisitiza kuwa, hakufahamu kuwa alizidisha kiwango hicho, na kwamba alikuwa na timu iliyohusika na kazi hiyo, kwa hivyo sio yeye aliyepaswa kulaumiwa.

Mbali na Sarkozy, watu wengine 13 kutoka katika chama chake cha kihafidhina cha republican, walihusishwa katika kesi hiyo na kukabiliwa na makosa ya kughushi, ukosefu wa uaminifu, ulaghai na ujumuishaji wa fedha haramu katika kampeni.

Miongoni mwao walipewa hukumu ya kifungo cha nje baada ya kukiri makosa yao na kuweka bayana mfumo wa risiti-bandia uliokuwa na lengo la kuficha matumizi makubwa ya kampeni hiyo.

Sarkozy alistaafu siasa za wazi mnamo mwaka 2017 lakini bado anaendesha majukumu yake nyuma ya pazia, kwa kuwa vyombo vya habari nchini Ufaransa vimeripoti kuwa anashiriki katika mchakato wa kumchagua mgombea atakaekiwakilisha chama chake kabla ya uchaguzi wa Urais nchini Ufaransa unaotarajiwa kufanyika mwakani.