1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia yathibitisha mazungumzo na Iran

7 Mei 2021

Afisa wa wizara ya mambo ya nje ya Saudi Arabia amesema mazungumzo na Iran yanalenga kuupunguza mzozo kati ya mahasimu hao wawili wa kikanda, lakini ameongeza kwamba ni mapema mno kuzungumzia matokeo.

https://p.dw.com/p/3t7Qb
Flagge Iran und Saudi-Arabien als Wandgemälde
Picha: daniel0Z/Zoonar/picture alliance

Matamshi yaliotolewa na balozi Rayed Krimly, mkuu wa mipango ya kisera katika wizara ya mambo ya nje ndiyo uthibitisho wa kwanza kutoka Saudi Arabia kwamba mahasimu hao waliovunja uhusiano mwaka 2016, walikuwa wanafanya mazungumzo.

Krimly aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa wanatumaini mazungumzo hayo yatadhihirisha ufanisi, na kwamba tathmini yao itategemea matendo yanayothibitika na siyo matamko.

Balozi Krimly hata hivyo amekataa kuingia kwa kina katika mazungumzo hayo, lakini maafisa wa kikanda na duru wameliambia shirika la Reuters kwamba majadiliano yamejikita juu ya Yemen na makubaliano ya nyuklia ya 2015 kati ya madola makubwa ya dunia na Iran, ambayo Riyadh iliyapinga.

Bildkombo | Mohammed bin Salman und Hassan Rohani
Mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, mwanamfalme Mohammed bin Salman (kushoto), na rais wa Iran Hassan Rouhani.

Rais wa Iraq alisema siku ya Jumatano kwamba Baghdad ilikuwa mwenyeji wa zaidi ya duru moja ya mazungumzo kati ya Saudi Arabia na Iran, ambazo zimekuwa na uhasama unaodhihirika katika vita vya uwakala katika kanda ya Mashariki ya Kati, ikiwemo nchini Yemen.

Soma pia: Iran yakaribisha mazungumzo na Saudi Arabia

Krimly alisema sera ya Saudia ilifafanuliwa kwa uwazi kabisaa na mrithi wa kiti cha Ufalme Mohammed Bin Salman, ambaye mwezi uliyopita alisema kwamba ingawa taifa hilo linalofuata madhebu ya Kisunni lilikuwa na tatizo la tabia hasi ya Tehran, lakini lilitaka kuwa na mahusiano mazuri na Iran inayoogozwa na Washia.

Vita nchini Yemen

Mzozo kati ya Riyadh na Tehran umeongezwa makali kuhusiano na vita nchini Yemen, ambako kundi la waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran limeongeza mashambulizi dhidi ya Saudi Arabia. Mvutano pia uliongezeka kufuatia shambulio la mwaka 2019 dhidi ya mitambo ya kuchakata mafuta ya Saudia, ambalo Riyadh ilililaumu kwa Iran, ingawa Tehran inakanusha.

Saudi iliunga mkono uamuzi wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump mwaka 2018 kuitoa Makrekani kwenye makubaliano ya nyuklia, kutokana na makubaliano hayo kutoshughulikia mpango wa makombora ya masafa marefu ya Iran. Baada ya Trump kurejesha vikwazo vikali dhidi ya Iran, Tehran ilijibu kwa kukiuka masharti kadha ya nyuklia.

Jemen I Schwere Gefechte in Sanaa
Vita nchini Yemen ni mmoja ya sababu zilizochochea mzozo kati ya Saudi Arabia na Iran.Picha: Hani Al-Ansi/dpa/picture alliance

Riyadh na Tehran pia zinaunga mkono pande zinazipingana nchini Lebanon na Syria, ambako Iran imemuunga mkono rais Bashar al-Assad. Mataifa ya Ghuba yamestushwa na kuongezeka kwa ushawishi wa mataifa yasio ya Kiarabu ya Iran, Urusi na Uturuki nchini Syria, hasa baada ya kusitishwa kwa uanachama wa Syria katika jumuiya ya mataifa ya Kiarabu mwaka 2011, kuhusiana na ukandamizaji dhidi ya waandamanaji mwanzoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Krimly amesema ripoti zakaribuni za vyombo vya habari kwamba mkuu wa shirika la upelelezi la Saudi Arabia alifanya mazungumzo mjini Damascus hazikuwa na ukweli. Amesisitiza kuwa sera ya Saudi Arabia kuelekea Syria inasalia kuwa na msingi wake kwenye uungaji mkono wa watu wa Syria, kwa ajili ya suluhisho la kisiasa chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa, na kulingana na maazimio ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, na kwa umoja na utambulisho wa Kiarabu wa Syria.

Chanzo: rtre