1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudia yaunga mkono juhudi za Marekani kwenye Mashariki ya Kati

6 Januari 2014

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry amesema Saudi Arabia imeonyesha nia ya kuziunga mkono juhudi za Marekani zinazoendelea za kusaka amani ya Mashariki ya Kati na kumaliza mzozo kati ya Israel na Palestina.

https://p.dw.com/p/1Alhv
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John KerryPicha: picture alliance / dpa

Kerry ametoa kauli hiyo baada ya kufanya mazungumzo na Mfalme Abdullah wa Saudia, mjini Riyadh jana Jumapili katika siku yake ya nne ya ziara katika Mashariki ya Kati. Mwaka 2002, Mfalme Abdullah alianzisha mpango wa kusaka amani kati ya Israel na Palestina. Kerry ameelezea mpango huo umekuwa sehemu ya mchakato ambao Marekani unauweka pamoja katika kupata ufumbuzi wa mzozo wa Mashariki ya Kati.

Pia Kerry ameelezea matumaini yake ya kufikiwa kwa makubaliano kati ya Israel na Palestina na kwamba masuala muhimu yaliyobakia yatapatiwa ufumbuzi hivi karibuni na kwamba makubaliano yatakayofikiwa yatakuwa ya haki kwa pande zote mbili.

Katika mikutano yake na Mfalme Abdullah wa Saudia, pamoja na mkutano wa awali na Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan, mjini Amman, Kerry aliwaelezea wafalme hao kuhusu mazungumzo aliyoyafanya na viongozi wa Palestina na Israel katika ziara yake ya siku tatu.

Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia
Mfalme Abdullah wa Saudi ArabiaPicha: AP

Kerry amshukuru Mfalme Abdullah wa Saudia

Akizungumza na waandishi wa habari, Kerry alisema anamshukuru sana Mflame Abdullah wa Saudia kwa kuonyesha nia yake ya kuunga mkono juhudi za kusaka amani ya Mashariki ya Kati na kwamba kiongozi huyo anaamini kuwa mpango wa amani unaweza ukaleta manufaa makubwa katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

Mazungumzo ya kusaka amani ya Mashariki ya Kati yanayosimamiwa na Marekani, yalianza tena mwezi Julai jana baada ya kukwama kwa miaka mitatu, huku Kerry akishinikiza kufikiwa kwa makubaliano ndani ya miezi tisa, licha ya pande zote mbili kuonyesha wasiwasi. Awali Kerry aliisihi Israel kuufikiria upya mpango wa amani wa mwaka 2002 uliopendekezwa na Mfalme Abdullah wa Saudia ambao unaitambua kamili Israel na kuitaka nchi hiyo kuirejesha ardhi inayoikalia kimabavu tangu mwaka 1967 na kutafuta ufumbuzi wa wakimbizi wa Kipalestina.

Kerry halikadhalika alikuwa na mazungumzo na waziri mwenzake wa Saudia, Mwanamfalme Saud al-Faisal, ambaye alisema mkutano baina yao unapuuzia taarifa zinazotolewa kwenye vyombo vya habari kwamba kuna mvutano kati ya Marekani na Saudi Arabia na kusema kuwa mkutano wao umekuwa mzuri. Mawaziri hao walizungumzia pia masuala mengine kadhaa ikiwemo mzozo wa Syria, Lebanon na Yemen.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia, Mwanamfalme Saud al-Faisal
Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia, Mwanamfalme Saud al-FaisalPicha: Fayez Nureldine/AFP/Getty Images

Kerry ambaye alirejea mjini Jerusalem jana jioni, alisisitiza kuwa anazihakikishia pande zote kwamba Rais Barack Obama wa Marekani pamoja na yeye mwenyewe wameweka mbele masuala ambayo ni ya haki, yasiyoegemea upande wowote ule na yenye kuimarisha usalama wa watu wote wa eneo la Mashariki ya Kati.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE,DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman