Jamhuri ya Afrika ya Kati yatuhumiwa kuandama wapinzani
4 Aprili 2023Kwa mujibu wa ripoti iliyosambazwa na shirika hilo siku ya Jumanne (Aprili 4), vyombo vya dola, ikiwemo polisi, vimekuwa vikiwatisha wanaharakati wa asasi za kijamii, vinaowatuhumu kushirikiana na makundi yenye silaha, na vinazuwia maandamano ya vyama vya upinzani.
Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Lewis Mudge, aliwaambia waandishi wa habari kwamba "kwa kufanya hivyo, serikali inayavunja kabisa matumaini ya kuwa na taifa linaloheshimu haki za binaadamu lililoahidiwa na katiba mpya ya mwaka 2016."
Soma zaidi:HRW: SCC mwanzo wa haki Afrika ya Kati
"Wakati uchaguzi unakaribia, Rais Faustin-Archange Touadéra anapaswa kuwapa majibu muafaka wakosoaji na kusaka njia za kushirikiana nao badala ya kuwashambulia." Alisema mkurugenzi huyo.
Vitisho vimeongezeka
Utafiti uliofanywa na shirika hilo unaonesha kuwa shinikizo na vitisho dhidi ya wapinzani wa kisiasa na wajumbe wa asasi za kijamii umeongezeka wakati uchaguzi wa wabunge wa Julai mwaka huu ukikaribia.
Wafuasi wa Rais Touadéra na washirika wao wa muungano unaotawala wa United Hearts Party (MCU) wamekuwa kwenye kampeni ya chini kwa chini ya kufanyika kura ya maoni ili kurekebisha katiba na kumruhusu kiongozi huyo kuwania kwa muhula wa tatu ifikapo mwaka 2025.
Soma zaidi: HRW: Kuna ushahidi wa mateso Jamhuri ya Afrika ya Kati
Wakati mdahalo juu ya kura hiyo ya maoni ukipamba moto, serikali inatumia taasisi zake kuvizuwia vyama vya upinzani kufanya mikutano ya kupinga mabadiliko hayo, huku ikiwaunga mkono wafuasi wa kambi inayoyaunga mkono kufanya mikutano yao na hata kuwapa ulinzi wa polisi
Human Rights Watch inasema kwa kufanya hivyo, "serikali inavunja haki ya msingi ya kuandamana kwa amani inayolindwa na katiba ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na sheria za kimataifa."
Waandishi, wanaharakati waishi kwa khofu
Baina ya mwezi Januari na Februari mwaka huu, Human Rights Watch inasema iliwahoji waandishi 30 wa habari, wanaharakati wa haki za binaadamu, wapinzani wa kisiasa, na maafisa wa kibalozi na serikali kwenye mji mkuu, Bangui.
Waandishi wa habari na wanaharakati walisema wamekuwa wakisita kuikosowa serikali ili kukwepa kuonekana wapinzani wa kisiasa na kutishiwa maisha yao na serikali.
Human Rights Watch imegunduwa kuwa jumuiya mbili zinazohusiana na muungano wa unaotawala wa MCU, kwa majina ya Requins na Galaxie Nationale, yanapiga kampeni ya kuunga mkono kura ya maoni na kuwashambulia wapinzani, mitaani na mitandaoni.