Shule zafungwa Ufaransa kutokana na kunguni
7 Oktoba 2023Mapema wiki hii, mamlaka ya Paris ilitangaza kufungwa kwa shule mbili kwa sababu ya kunguni, moja huko Marseille na nyingine Villefranche-sur-Saone nje kidogo ya mji wa kusini mashariki wa Lyon.
Serikali ya Ufaransa imefanya msururu wa mikutano wiki hii kuchunguza idadi inayoongezeka ya visa vya kunguni, wakati nchi hiyo ikiandaa Kombe la Dunia la Rugby na ambayo itakuwa mwenyeji ya Michezo ya Olimpiki hapo mwakani.
Serikali mjini Paris imelazimika sasa kuingilia kati kupambana na kunguni hao. Ijumaa iliyopita, Waziri Mkuu wa Ufaransa Elisabeth Borne aliitisha kikao cha baraza la mawaziri kujadili namna ya kupambana na kunguni.
Waziri wa Usafiri Clement Beaune alikutana wiki hii na makampuni ya usafirishaji kubuni mpango wa kufuatilia na kunyunyizia dawa vyombo vya usafiri wa umma na, yumkini, kujaribu kupunguza wasiwasi wa nchi nzima uliochochewa zaidi na vyombo vya habari.
Baada ya taarifa kuwa kunguni walipatikana kwenye jengo la sinema mwezi mmoja uliopita, raia wa Ufaransa walianza kusambaza video katika mitandao ya kijamii zikionesha wadudu hao wakitambaa majumbani na kwenye usafiri wa umma kama matreni na mabasi.
Kunguni wavamia sehemu mbalimbali Ufaransa
Kunguni wamekuwepo Ufaransa na mataifa mengine ya Ulaya kwa miongo kadhaa na hakuna mwenye kinga ya kuvamiwa na wadudu hao. Mtaalamu wa vidudu kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Mediterenia mjini Marseille, Ufaransa, Jean-Michel Berenger, anasisitiza kuwa kunguni hawatokani na uchafu, bali wanachofuata ni damu ya mtu.
Maktaba moja ya manispaa katika mji wa kaskazini wa Amiens inatazamiwa kufunguliwa tena siku ya Jumamosi baada ya kufungwa kwa siku kadhaa baada ya kunguni kugunduliwa katika maeneo ya kusomea vitabu, amesema meya wa jiji hilo Brigitte Foure akisisitiza kuwa mbwa wa kunusa hawakugundua uwepo wowote wa wadudu hao baada ya maktaba hiyo kushughulikiwa.
Takwimu za Shirika la Afya na Usalama wa Chakula nchini Ufaransa zinaonesha kuwa angalau nyumba moja kati ya kumi nchini humo ilikuwa na kunguni katika miaka michache iliyopita. Kuwatokomeza kunguni inagharimu pesa nyingi na wakati mwingine zoezi hilo hurudiwa mara kadhaa.
Kunguni wameripotiwa sehemu mbalimbali nchini Ufaransa kama kwenye treni za mwendo kasi katika mji mkuu Paris, na hata katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Charles De Gaulle.
Kunguni ni mdudu mdogo asiyeweza kuruka bali anayeweza kutembea haraka kutoka sehemu moja hadi nyingine au hata nchi hadi nchi, na imekuwa vigumu kumtokomeza kwa kutumia dawa za kuulia wadudu. Lakini pia, kunguni anaweza kuishi hata mwaka mzima bila kula.
(AFPE)