1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSierra Leone

Sierra Leone yatangaza amri ya kutotoka nje

Sylvia Mwehozi
26 Novemba 2023

Sierra Leone imetangaza amri ya nchi nzima ya kutotoka nje baada ya watu wasiojulikana waliojihami kwa silaha kushambulia kambi moja ya kijeshi katika mji mkuu wa Freetown.

https://p.dw.com/p/4ZSFe
Sierra Leone | Freetown
Maafisa wa usalama mjini Freetown nchini Sierra Leone wakishika doriaPicha: Umaru Fofana/REUTERS

Sierra Leone imetangaza amri ya nchi nzima ya kutotoka nje baada ya watu wasiojulikana waliojihami kwa silaha kushambulia kambi moja ya kijeshi katika mji mkuu wa Freetown.

Taarifa iliyotolewa na waziri wa habari wa Sierra Leone Chernor Bah, imesema kwamba "katika majira ya asubuhi ya siku ya Jumapili, watu wasiojulikana walijaribu kuingia katika ghala la kijeshi kwenye kambi ya Wilberforce."

Waziri huyo ameongeza kuwa watu hao wamefurushwa na kutoa wito kwa umma kusalia nyumbani. "Amri ya nchi nzima ya kutotoka nje imetangazwa mara moja. Tunawashuri watu kusalia ndani", ilisema taarifa hiyo.

Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio pia ametoa hakikisho kwamba utulivu umerejeshwa katika mji mkuu wa Freetown, akiwataka watu kusalia majumbani.

Sierra Leone | Julius Maada Bio
Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio Picha: Cooper Inveen/REUTERS

"Ili kuwezesha vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea na msako dhidi ya washukiwa, amri ya kutotoka nje inatangazwa mara moja kote nchini," amesema Rais Maada Bio.

Sierra Leone yafanya Uchaguzi Mkuu

Ameongeza kuwa serikali "itaendelea kulinda amani na usalama wa Sierra Leone dhidi ya vikosi vinavyotaka kuvuruga utulivu wetu unaothaminiwa sana."

Hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa juu ya wanaodaiwa kuhusika na shambulio hilo, au dhamira yao.

Mashuhuda wasimulia milio ya risasi

Awali, mashuhuda walilieleza shirika la habari la AFP kuwa walisikia milio ya risasi na milipuko katika wilaya ya Wilberforce mjini Freetown, kunakopatikana ghala hilo la silaha pamoja na balozi kadhaa za kigeni.

Shuhuda mwingine alisema kuwa alisikia mabadilishano ya risasi karibu na kambi ya kijeshi kwenye wilaya ya Murray kwenye kambi ya jeshi la wanamaji, sambamba na nje ya kambi nyingine ya kijeshi huko Freetown.

Bofya hapa kusoma hii habari: Sierra Leone yapiga marufuku mikutano ya kisiasa mitaani

Mitaa ya mji huo ilikuwa mitupu kwa mujibu wa mashuhuda.

Afisa mmoja mwandamizi ambaye aliomba kutotajwa jina alilieleza shirika la habari la Reuters kwamba gereza kuu la Freetown lilikuwa wazi na baadhi ya wafungwa walitoroka.

Hali ya kisiasa katika taifa hilo la Afrika Magharibi imesalia kuwa ya wasiwasi tangu kuchaguliwa tena kwa Rais Julius Maada Bio katika uchaguzi uliokumbwa na utata mwezi Juni, ambao matokeo yake yalikataliwa na mgombea mkuu wa upinzani.

Wanajeshi wa Sierra Leone mwaka 2000
Wanajeshi wa Jeshi la Sierra Leone wakikusanyika baada ya kuuteka tena mji wa Masiaka kutoka kwa waasi wa Revolutionary United Front (RUF) tarehe 13 Mei 2000.Picha: Issouf Sanogo/AFP

Soma kuhusu uchaguzi wa Sierra Leone: Rais wa Sierra Leone aongoza matokeo ya uchaguzi

Maandamano ya kupinga serikali ambayo yalisababisha vifo vya maafisa sita wa polisi na raia wasiopungua 21 Agosti mwaka jana, yalikuwa ni jaribio la kupindua serikali, kwa mujibu wa Rais Maada Bio.

Kumekuwa na mapinduzi 8 ya kijeshi katika kanda ya Afrika Magharibi na Kati tangu mwaka 2020, hali inayodhoofisha demokrasia katika eneo hilo. Mali, Burkina Faso, Niger na Guinea, ambayo inapakana na Sierra Leone, zote zimeangukia chini ya udhibiti wa kijeshi.Mataifa ya Afrika ya Kati yachukulia vipi mapinduzi Gabon ?

Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, imelaani kile ilichokiita jaribio la watu fulani "kuchukua silaha na kuvuruga utaratibu wa kikatiba" nchini Sierra Leone. Nao ubalozi wa Marekani mjini Freetown umesema katika taarifa yake kwamba vitendo kama hivyo haviikubaliki.

Vyanzo: Reuters/AFP