Tetemeko la ardhi Morocco: Idadi ya vifo yakaribia 2,900
12 Septemba 2023Idadi ya vifo inazidi kuongezeka na hadi sasa imefikia karibu watu 2,900 huku wengine zaidi ya 2,500 wakiwa wamejeruhiwa. Vikosi vya uokoaji vimeendelea bila kuchoka kuwatafuta manusura, lakini katika kijiji cha Tafeghaghte, ni hali ya huzuni ndio iliyotawala jioni ya siku ya Jumatatu ambapo miili ya nusu ya wakazi wapatao 160 ilipatikana.
Juhudi za vikosi vya uokoaji zimeshuhudiwa katika maeneo mbalimbali yaliyokumbwa na janga hilo ambapo askari wa Morocco kwa ushirikiano na mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka Mataifa ya Uhispania, Qatar, Uingereza na Falme za Kiarabu yamekuwa yakifanya kazi usiku kucha na kutoa huduma muhimu na za haraka kwa manusura.
Morocco imekuwa ikikosolewa kuchelewesha kutoa idhini kwa mashirika mengine ya uokoaji kuingia nchini humo ili kutoa msaada wao, na maafisa wa Ufalme huo wanasema uamuzi huo unalenga kuepuka mkanganyiko katika uratibu ambao wanadai "hautokuwa na manufaa yoyote".
Mbinu hiyo ni tofauti na ile iliyochukuliwa na serikali ya Uturuki, ambayo ilitoa ombi la usaidizi wa kimataifa katika saa chache tu zilizofuata tetemeko kubwa la ardhi mapema mwaka huu, ambalo pia liliipiga nchi jirani ya Syria.
Mwanzilishi wa Kikosi cha waokoaji wasio na mipaka Arnaud Fraisse ameliambia shirika la habari la AP kuwa msaada zaidi ungeweza kuwasili haraka zaidi nchini Morocco ikiwa serikali ingelitoa ruhusa. Na kuongeza kuwa takriban timu zipatazo 100 zenye jumla ya waokoaji 3,000 tayari wamesajiliwa na Umoja wa Mataifa.
Ufaransa yatoa msaada kwa Morocco
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Catherine Colonna amesema Morocco ndio waamuzi na msimamo wao ni lazima uheshimiwe. Ufaransa imetangaza msaada wa dharura kwa Morocco wa dola milioni 5.4 utakaolekezwa kwa mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali yanayoendelea kutoa msaada nchini humo.
Hata hivyo Morocco ilitangaza kukubali msaada wa Algeria ambayo imetoa msaada wa ndege tatu za kusafirisha kikosi cha watu 93 wa idara ya uokozi pamoja na misaada mingine ya kibinaadamu.
Waziri Mkuu wa Morocco Aziz Akhannouch amekutana hapo jana na Mfalme wa Morocco Mohammed VI na kuhutubia kwa mara ya kwanza hadharani tangu kutokea kwa tetemeko hilo la ardhi. Akhannouch amesema nchi hiyo ya Afrika Kaskazini imedhamiria kufadhili kuijenga upya Morocco.
Kulingana na vyanzo vya kuaminika, serikali ya Morocco inalenga pia kuendelea mazungumzo na Benki ya Dunia pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa yaliyopangwa kufanyika mjini Marrakesh Oktoba 9 hadi 15, 2023. Lakini taasisi zote mbili zimesema kipaumbele kwa sasa ni kushughulikia kwanza maafa yaliyotokana na janga hilo.