Tetemeko la ardhi Morocco: Mamia waachwa bila makazi
11 Septemba 2023Juhudi za uokozi zimekuwa zikisuasua kutokana na miundombinu kama barabara kuharibiwa vibaya nchini humo. Hata hivyo vikosi vya uokoaji vimeendelea na zoezi gumu la kuwasaka manusura licha ya kutatizika kufika katika maeneo ya milimani. Manusura wengi wamekosa mawasiliano kutokana na kukatika kwa umeme na hasa simu zao zikiiishiwa chaji.
Brahim Edmu, mkazi wa mji wa Marrakesh amesema alikuwa akijaribu kuelekea katika moja wapo ya kijiji kichopo milimani cha Talat N'Yaaqoub, ambacho kiliathiriwa mno na tetemeko hilo la ardhi huko Al Haous, na kwamba yeye na marafiki wangeweza kutoa msaada, lakini barabara haipitiki kwa takriban kilometa 10 kutokana na maporomoko ya mawe. Shuhuda huyo amesema watu wengi eneo hilo bado wamefukiwa na vifusi.
Morocco imefahamisha siku ya Jumapili kuwa imeafiki msaada kutoka nchi za Uhispania, Qatar, Uingereza na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ambazo zitapeleka vikosi vya uokoaji.
Serikali ya Rabat imesema inaweza hapo baadaye kukubali usaidizi kutoka kwa mataifa mengine. Nchi kadhaa zimeonyesha kuguswa na kutangaza kuwa tayari kutoa msaada kwa Morocco . Wizara ya Ulinzi ya Uhispania umetuma kikosi maalum cha uokoaji kutoka jeshini chenye jumla ya watu 56 na mbwa wanne.
Mataifa mengine yasubiri kutoa msaada
Kikosi cha Uokoaji cha Ujerumani kimesema kiko tayari kutoa msaada wake kwa maelfu ya watu walioathiriwa na janga hilo.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema pia kuwa Ufaransa iko tayari kutoa msaada wake ikiwa serikali ya Rabat itaidhinisha hilo. Macron amesema mamilioni ya raia wa Ufaransa wenye asili ya Morocco walikuwa na familia katika mikoa iliyokumbwa na tetemeko kubwa la ardhi siku ya Ijumaa, na kuongeza kuwa janga hilo limewagusa mno watu nchini Ufaransa.
Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC) limesema waokoaji wa Hilali Nyekundu wa Morocco watapokea takriban dola milioni 1.1 ili kukabiliana na matokeo ya tetemeko kubwa la ardhi. Timu za Hilali Nyekundu za Morocco zimekuwa zikitoa misaada katika maafa kama vile huduma za kisaikolojia, utafutaji na hata uokoaji.
Umoja wa Mataifa umekadiria kuwa watu 300,000 wameathiriwa na tetemeko hilo la Ijumaa usiku lenye kipimo cha 6.8 na baadhi ya Wamorocco wamekuwa wakilamika katika mitandao ya kijamii kwamba serikali haikuwa ikiruhusu misaada zaidi kutoka nchi za nje.