1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi amshutumu Kabila kuunga mkono waasi

Sylvia Mwehozi
8 Agosti 2024

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi amemshutumu rais wa zamani Joseph Kabila kwa kuunga mkono muungano wa makundi ya waasi uliowekewa vikwazo na Marekani.

https://p.dw.com/p/4jBaw
Félix Tshisekedi na Joseph Kabila
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi (kushoto) na rais wa zamani Joseph Kabila(kulia)

Tshisekedi ametoa shutuma hizo wakati wa mahojiano na kituo binfasi cha redio jana Jumanne. Kiongozi huyo amenukuliwa wakati wa mahojiano hayo akisema kwamba Kabila alisusia uchaguzi na anapanga kuanzisha uasi kwasababu anaunga mkono muungano huo wa makundi ya waasi unaojulikana kama AFC.

Shutuma za Uganda: Rais wa Uganda Yoweri Museveni amedai kuwa utawala wa rais wa zamani wa Kongo Joseph Kabila uliwahifadhi waasi wa Uganda ADF mashariki mwa Kongo

Muungano huo unadaiwa kuwa vuguvugu la kisaisa na kijeshi ulioanzishwa mwezi Desemba kwa lengo la kuyaunganisha makundi yote yenye silaha, vyama vya siasa na asasi za kiraia dhidi ya serikali ya Kongo. Hata hivyo kiongozi huyo wa Kongo hakutoa ushahidi wowote kuhusu madai yake.

Shutuma hizo za Tshisekedi zinafuatia tangazo la Marekani la kuuwekea vikwazo muungano wa AFCmwezi uliopita. Washington inaushutumu muungano huo kwa kujaribu kuipindua serikali ya Kongo na kuchochea mzozo mashariki mwa nchi.

Tshisekedi: Amani imo mikononi mwa rais atakayemrithi Kagame

Marekani ilisema kuwa mwanachama mkuu katika muungano huo kundi la waasi wa M23tayari liko chini ya vikwazo vya Washington. Tshisekedi, pamoja na wataalamu wa Marekani na Umoja wa Mataifa, wanaishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kulisaidia kijeshi kundi la M23.

Rwanda inakanusha madai hayo, lakini mwezi Februari ilikiri kwamba ina wanajeshi na mifumo ya makombora mashariki mwa Kongo ili kulinda usalama wake, ikitaja ongezeko la vikosi vya Kongo karibu na mpaka.

Kongo na Rwanda wiki iliyopita zilikubaliana kusitisha mapiganoambayo yalianza Jumapili kufuatia mazungumzo yaliyopatanishwa na Angola.

Eneo la Mashariki mwa Kongo limekuwa likikabiliwa na ghasia huku zaidi ya makundi 120 yakipigania udhibiti wa ardhi na rasilimali muhimu za madini, na mengine yakijaribu kutetea jamii zao. Soma pia: Rais wa zamani wa Kongo Kabila awataka wafuasi kupinga udikteta

Baadhi ya makundi yenye silaha yamekuwa yakituhumiwa kwa mauaji ya halaiki. Machafuko yaliyokithiri mashariki mwa jimbo la Kivu Kaskazini sio tu yamesababisha mauaji ya kiholela bali pia unyanyasaji wa kingono.