Uchunguzi: Waathiriwa tetemeko Uturuki na tishio la saratani
27 Septemba 2023Kwenye mji wa Hatay, kusini mwa Uturuki hadi sasa makundi ya wafanyakazi bado wanabomoa mabaki ya majengo yaliyoharibiwa au kuondoa vifusi vya yale yaliyoporomoshwa na tetemeko la kutisha la ardhi lililotokea mwezi Februari.
Wafanyakazi waliovalia vizibao vya manjano kila siku wanahamisha rundo la vifusi na kutibua vumbi jingi linalotandaa mji mzima.
Watoto wa mji huo wanatembea juu ya vifusi hivyo hivyo wakitafuta mahala pa kucheza kabumbu na wakiwa kwenye harakati hizo huenda wanavuta hewa iliyochanganyika na asbestos, madini yaliyothibitisha kuwa hatari kiafya na yaliyopachikwa jina la "muuaji wa kimya kimya".
Soma pia:UN yachangisha robo ya fedha za msaada kwa Uturuki kufuatia tetemeko la ardhi
Uchunguzi uliofanywa na waandishi wa DW umebaini bila kificho kuwa viambata vya madini ya asbestos vimetapakaa kila sehemu ya mji huo tangu kwenye mimea, udongo na hata vifusi.
Hali hiyo inatishia kuleta balaa kubwa la kiafya kwenye eneo hilo lenye shughuli nyingi za kilimo.
Matokeo ya uchunguzi katika vifusi
Kikosi cha wataalamu kutoka asasi ya ulinzi wa mazingira nchini Uturuki kilikusanya sampuli za vumbi kutoka mji wa Hatay ambazo baadaye zilifanyiwa uchunguzi wa kina na maabara yenye viwango vinavyosifika kimataifa ya AGT Vonka kwa ajili ya waandishi wa DW.
Uchunguzi wao umebaini bila ya shaka uwepo wa viambata vya asbestos kwenye mji huo licha ya maafisa wa serikali kukataa matokeo hayo.
Wataalamu wa afya ya umma wameimbia DW kuwa watu wanaoishi kwenye eneo hilo lililoathiriwa na tetemeko la ardhi ikijumuisha maelfu ya watoto, wamo kwenye hatari ya kupata saratani zinazofungamanishwa na madini asbestos ikiwemo ya mapafu na ile vilango vya kupitisha hewa mwilini.
"Katika miaka inayokuja, tutashuhudia vifo vya makumi kwa maelfu ya vijana."
Alisema daktari Ozkan Kaan Karadag, mtaalamu wa masuala ya afya aliyetizama matokeo ya uchunguzi wa maabara uliofanywa kwa maombi ya waandishi wa DW.
Soma pia:Miezi sita baada ya tetemeko kubwa la ardhi huko Syria na Uturuki
Aliongeza kwamba madhara hayo kwa wakaazi ni kutokana na kuvuta hewa ambayo tayari imechafuta.
Usafishaji wa mabaki na taka za baada ya tetemeko zinaitumbukiza jamii nzima ya wakaazi wa Hatay kwenye kitisho cha matatizo ya kiafya.
Madini ya asbestos yaliyosifika hapo kale kama malighafi ya kimapinduzi kwenye sekta hasa ya ujenzi hivi sasa yameorodheshwa kuwa miongoni mwa yale hatari zaidi duniani. Tathmini hiyo ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO.
Malighafi hiyo ilitumika kwa muda mrefu kwenye sekta ya ujenzi kutokana na uwezo wake wa kudhibiti moto na kumomonyoka kwa kuta za majengo au vifaa vingine vilivyotumika kwenye ujenzi.
Uturuki bado inatumia madini ya asbestos?
Nchini Uturuki, asbestos bado inapatikana kwa wingi kwenye majengo mengi yaliyojengwa kabla ya marufuku iliyotangazwa mwaka 2010.
Pindi majengo au vifaa vilivyopakazwa asbestos vinapoharibika au kusambaratika hususani kwenye paa, kuta na mtandao wa umeme kwenye majumba basi madini hayo hunyambuka na kuwa viambata vidogosana vinavyowezwa kutapakaa kwenye hewa na kusafirishwa kwa upepo.
Mashirika kadhaa nchini Uturuki ikiwemo muungano wa wahandisi na wasanifu majengo nchini humo wamesema tahadhari wanayoitoa kwa mamlaka juu ya kitisho cha asbestos kwenye majengo yaliyoporomoka haitiliwi maanani na viongozi.
Badala yake viongozi wanapuuza mfano ikiwa ni aliyekuwa naibu waziri wa mazingira na ukuzaji miji wa Uuturuki Mhemet Emin Birpinar alikanusha mwezi Juni akisema hakuna viambata vya asbestos kwenye anga ya miji ya Uturuki.
Soma pia:Waliokufa jkwa tetemeko Uturuki wafikia 50,800
Aliandika mtandaoni kuwatoa shaka wakaazi katika eneo hilo klililokubwa na tetemeko kwamba wapo salama.
"Raia wetu kwenye eneo lililokumbwa na tetemeko la ardhi wawe na uhakika kuwa tunafanyia kazi kwa umakini suala la asbestos."
Lakini uchunguzi wa DW kupitia sampuli 45 zilizokusanywa kutoka maeneo yaliyokumbwa na tetemekondani ya mji wa Hatay na vitongoji jirani zinapingana na msimamo wa serikali.
Saratani zitokanazo na asbestos mara nyingi huchukua miaka kadhaa kutokea na hilo ndiyo linawafanya wataalamu huru nchini Uturuki wapaze sauti.
Wanashinikiza mamalaka kukiri kuwa tatizo hilo lipona wajibu wa mamlaka za nchi hiyo ni kutoa ulinzi na kupendekeza njia salama na kujikinga na madini hayo hatari.