1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 1000 wanusurika kwenye shambulio la makombora

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
28 Juni 2022

Waokoaji wanaendelea kuwatafuta watu kwenye kifusi baada ya eneo la maduka kushambuliwa katika jiji la Kremenchuk nchini Ukraine siku ya Jumatatu mchana. Takriban watu 18 wameuawa na wengi wamejeruhiwa.

https://p.dw.com/p/4DM6n
BG Angriff auf Einkaufszentrum in Krementschuk
Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amelitaja shambulio hilo kuwa ni moja ya mashambulizi ya magaidi ya kikatili katika historia ya Ulaya. Zelensky ameelezea kwamba ni bahati kubwa kwambva wengi kati ya wanunuzi zaidi ya 1,000 na wafanyikazi ndani ya maduka katika jiji hilo la Kremenchuk walifanikiwa kukimbia.

Moshi mkubwa na miale ya rangi ya chungwa ya moto bado imetanda kwenye mabaki ya jumba hilo lililokuwa na maduka huku wafanyakazi wa dharura wakipekua  kwenye kifusi kuwatafuta watu walioathiriwa kwenye mkasa huo. Ndege zisizo na rubani zilizunguka juu angani, kwenye wingu la moshi mweusi saa kadhaa baada ya moto huo kuzimwa.

Moshi mzito katika eneo la maduka kwenye jiji la Kremenchuk baada ya kushambuliwa kwa makombora.
Moshi mzito katika eneo la maduka kwenye jiji la Kremenchuk baada ya kushambuliwa kwa makombora.Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Soma pia: Kombora la Urusi lawauwa watu 16 madukani Ukraine

Oleksandr Chernysh, mfanyakazi wa shirika la Msalaba Mwekundu mjini Kiyv anayeshiriki kwenye zoezi la uokozi ameeleza kuwa baadhi ya watu waliokolewa wamejeruhiwa kwenye shambulio hilo na wengine wamepata mshtuko. Amesema baadhi ya watu walioumia ni wazee ambao wamevunjika mifupa kwenye sehemu mbalimbali miilini mwao na hali hiyo inawasababishia ugumu sana kutokana na umri wao ikilinganishwa na vijana.

Gavana wa mkoa wa kati wa Poltava, nchini Ukraine, Dmytro Lunin, amesema watu 36 bado wanazingatiwa kutoweka baada ya shambulio la kombora la Urusi kwenye duka hilo kubwa katika jiji la Kremenchuk. Ukraine inailaumu Urusi kwa kufanya shambulio hilo lililolenga eneo ambalo liko mbali na mstari wa mbele wa vita.

Soma pia: Viongozi wa G7 waapa kuisaida Ukraine "bila kuchoka"

Urusi imekanusha kuwalenga raia kimakusudi kwenye operesheni yake maalum ya kijeshi. Wizara ya ulinzi ya Urusi leo imesema jeshi lake lilirusha makombora kulenga ghala la silaha katika mji huo wa Kremenchuk, na mlipuko ulitokea kutokana na kuwepo silaha katika eneo hilo ambazo zilisababisha moto huo mkubwa katika eneo la maduka ambalo lilikuwa karibu na ghala hilo la silaha.

Urusi pia imeeleza kuwa maduka makubwa katika eneo hilo la Kremenchuk yalikuwa yamefungwa kutokana na mgomo ulikokuwepo siku ya Jumatatu.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: ROSLAN RAHMAN/AFP

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambapo Urusi ni mwananchama mwenye kura ya turufu, litakutana leo Jumanne kwa ombi la Ukraine kufuatia shambulio hilo. Msemaji wa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema shambulio hilo la kombora dhidi ya eneo la raia ni kitendo cha kusikitisha.

Soma pia: Hali ngumu Lysychansk Ukraine

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema amemwambia Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg kwenye mazungumzo yao kwa njia ya simu kwamba nchi yake inahitaji mifumo ya ulinzi wa makombora ili kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Urusi.

Vyanzo:RTRE/AFP/DPA/AP