Umoja wa Mataifa wataka Myanmar iondolewe vikwazo
30 Aprili 2012Katibu Mkuu huyo amezungumza hayo alipolihutubia bunge la nchi hiyo leo, sehemu ya ziara yake ya siku tatu nchini Myanmar. Hotuba hiyo aliitoa baada ya mazungumzo yake na Rais Thein Sein.
Ki-moon aliliambia bunge hilo kwamba anakaribisha jitihada za jumuiya za kimatiafa huku akisema vitendo zaidi katika kufanikisha ustawi wa Myanmar vinahitajika.
Alisisitiza kwamba jamii za kimataifa zinapaswa kuondoa, kusimamisha au kulegeza vikwazo vya kibiashara pamoja na vinginevyo ili taifa hilo lisonge mbele.
Kiongozi huyo pia anatarajiwa kukutana na kiongozi wa upinzani nchini humo Aung San Suu Kyi, katika ziara yake hiyo ya kwanza kuifanya tangu taifa hilo lililokuwa likijulikana kama Burma kuhitimisha utawala wa kijeshi ambao ulidumu kwa miongo kadhaa.
Hata hivyo Suu Kyii hakuwepo bungeni wakati Ki moon akihutubia bunge kwa kuwa kiongozi huyo na wenzake kadhaa walikuwa katika mgomo wa kupinga vifungu vya katika ya nchi hiyo.
Awali katika mazungumzo yake na rais Thein Sein katibu mkuu wa umoja wa mataifa ofisi yake itasaidia taifa hilo kufanikisha sensa ya kwanza kufanyika kwa kipindi cha miaka 31.
Miongoni mwa maeneo ambayo watasaidia ni pamoja na ufundi na kuwezesha upatikanaji wa fedha. Rais Thein Sein ambae ni mkuu wa jeshi wa zamani ameonesha nia ya kufanikisha mabadiliko nchini humo tangu aingie madarakani.
Miongoni mwa mambo muhimu aliyoweza kuyafanya ni pamoja na kuruhusu chama cha siasa cha upinzani kinachoongozwa na mwanaharakati Suu Kyi pamoja na kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa.
Pamoja na mambo mengine kwa upande wake Ban Ki-moon anatarajiwa kuitaka mamlaka ya taifa hilo kuruhusu misaada ya kibinadamu ya umoja mataifa kwa maelfu ya wakimbizi waliotokana na mapigano kati ya wanajeshi na kabila dogo lililoasi katika jimbo la kaskazini ya mbali la Kachin.
Pamoja na Umoja wa Mataifa kufanikiwa kutuma ujumbe wake wa usaidizi katika eneo hilo hivi karibuni lakini bado watu wengi wameendelea kuishi katika mkwamo mkubwa huku hali hiyo ikitabiriwa uenda ikawa mbaya zaidi.
Sambamba na yanayotokea sasa Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu kabisa katika Umoja wa Ulaya Catherine Ashton nae yupo Myanmar kwa ajili ya mazungumzo na rais wa taifa hilo baada ya umoja huo kusimamisha vikwazo vyake dhidi ya taifa hilo .
Mwandishi: Sudi Mnette/ AFP
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman