UN, washirika wa Somalia wawataka viongozi kutatua mzozo
30 Desemba 2021Kwa mujibu wa afisa wa serikali ya Somalia, waziri mkuu Mohammed Hussein Roble amefanya mazungumzo tofauti na naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Afrika, Molly Phee, kuhusu hali ya kisiasa nchini Somalia, hali ambayo wachambuzi wanasema inavuruga juhudi za serikali za kupambana na waasi wa kundi la Al-Shabaab.
Ofisi ya Phee ilisema kupitia mtandao wa Twitter kwamba, alikuwa amezungumza pia na rais Mohamed Abdullah Mohamed, na kumuhimiza kumuunga mkono Roble ili akamilishe uchaguzi wa bunge haraka.
Uchaguzi huo ulianza Novemba 1, na ulipaswa kukamilishwa kufikia Desemba 24, lakini kufikia Jumatano, ni wawakilishi 30 tu kati ya 275 walikuwa wamechaguliwa, kulingana na tume ya uchaguzi.
Soma pia: Washirika wa Somalia waelezea wasiwasi wa mzozo wa kisiasa
Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Ari Gaitanis, amesema umoja huo na washirika wake wa kimataifa wanawasiliana na pande zote kuzihimiza kupunguza mzozo. Kwa mujibu wa Gaitanis, mazungumzo hayo yanahusisha washirika wa UN nchini Somalia, wanaojumlisha Marekani, Uingereza, Umoja wa Ulaya na wengine.
Rais wa Somalia Mohamed, alitangaza kumsimamisha kazi waziri mkuu siku ya Jumatatu, kwa shutuma za rushwa, hatua ambayo Roble aliilinganisha na jaribio la mapinduzi na kuvitaka vikosi vya usalama kuchukua amri kutoka ofisi yake.
Al-Shabaab yateka mji
Kila mmoja anamlaumu mwenzake kwa kuwa chanzo cha ucheleweshaji unaoshuhudiwa katika mchakato wa uchaguzi. Lakini mkaazi wa Mogadishu Abdijamal Hajji, anamlaumu rais Mohamed kwa kuwa chanzo cha yote hayo.
"Msuguano ndani ya serikali siyo kitu kizuri, mabishano hayo ya kisiasa kati ya rais wa zamani na kaimu waziri mkuu umeathiri maelfu ya Wasomali. Rais alichaguliwa kidemokrasia, na nilikuwa moja wa wafuasi wake, lakini baadae nilijutia kumuunga mkono kwa sababu alisababisha matatizo mengi," alisema mkaazi huyo.
Soma pia: Viongozi kuharakisha mchakato wa uchaguzi Somalia
Wakati viongozi hao wawili wakidi kuvutana, polisi na wakaazi katika mji wa Balad ulioko kilomita 30 kaskazini mwa Mogadishu, wamesema wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab lenye mafungano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, wameukamata mji huo baada ya kufanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya serikali vilivyokuwa vinalinda daraja la kuingilia mjini humo leo asubuhi.
Kapteni wa polisi Farah Ali amesema, baada ya kuuteka mji wa Balad, wapiganaji wa Al-Shabaab walikaa kidogo na kisha kuondoka bila kufanya doria,katika shambulio hilo watu wasiopungua nane wamekufa, wakiwemo wanajeshi wa serikali.
Chanzo: rtre, aptn