1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNHCR: Wahamiaji wanyanyaswa na maafisa wa Afrika

29 Julai 2020

Ripoti mpya ya UNHCR kuhusu wahamiaji ambao hufanya safari ndefu na kupitia njia hatari, imebaini kuwa takriban nusu ya dhuluma walizokumbana nazo zilifanywa na maafisa wa serikali katika nchi za Afrika walikopitia.

https://p.dw.com/p/3g88V
Libyen Migranten an der Küste bei Khoms
Picha: Getty Images/AFP/M. Turkia

Ripoti hiyo ambayo inatarajiwa kuibua miito ya uwajibikaji mkubwa, imetolewa Jumatano Julai 29 na shirika la UNHCR pamoja na Baraza la Uholanzi kuhusu Wahamiaji.

Kusudi la ripoti hiyo lilikuwa kuorodhesha matukio ya dhuluma na maafa ambayo yamekuwa vigumu kufuatilia katika njia za kuelekea Ulaya wahamiaji wakivuka kati ya Libya kuelekea Ulaya huku wakijaribu kukwepa kupitia bahari ya Mediterrania.

Ripoti hiyo yenye kichwa 'Katika safari hii, hakuna anayejali ukiishi au ukifa' pia inaonya kwamba janga la COVID-19 ambalo limesababisha mipaka ya nchi kufungwa, linaweza kufanya safari hizo kuwa hatari hata zaidi, mnamo wakati wanaofanya biashara haramu ya kusafirisha watu kinyume cha sheria wakijaribu kutumia mbinu hatari zaidi za kuepusha kugunduliwa.

Takwimu ni chini ya idadi kamili ya vifo

Kwa kuzingatia watu 16,000 waliohojiwa pamoja na data zilizokusanywa na Kituo cha Uhamiaji Mchanganyiko, ripoti hiyo ilibaini kuwa takriban watu 1,750 walifariki wakiwa katika safari hizo hatari kutoka Afrika Mashariki na pia Afrika Magharibi katika miaka ya 2018 na 2019. Hali hii inafanya safari ya ardhini kuwa miongoni mwa njia hatari zaidi kwa wahamiaji ulimwenguni.

Libyen Auffanglager für Flüchtlinge in Zawiya bei Tripolis
Wahamiaji wa Kiafrika wakiwa katika kituo cha uzuwiaji mjini Zawiya, magharibi mwa Tripoli, kufuatia mapigano kati ya vikosi vya serikali hasimu nchini humo.Picha: Getty Images/AFP/M. Turkia

Shirika la UNHCR linaamini kwamba takwimu hiyo imepungua idadi kamili ya vifo.

"Tumekuwa tukipata ripoti kadhaa kwamba kumekuwa na manyanyaso njiani yanayofanywa na maafisa wa usalama, au walanguzi na wasafirishaji haramu wa wanadamu." Alisema Vincent Cochetel ambaye ni mjumbe maalumu wa shirika la UNHCR katika Mediterrania ya Kati.

Soma kuhusu Madhila wanayopitia watoto wakimbizi wanaowasili Uganda

"Sasa tuna taarifa ya kina kuhusu ni wapi madhila hayo yanafanywa na yanatendwa na nani. Kwa hivyo hakuna anayeweza kusema hatujui.'' Aliongeza kusema Vincent.

Maafisa wa usalama waongoza udhalilishaji

Ripoti ilibaini kwamba asilimia 47 ya visa vya manyanyaso ya kimwili yaliyoripotiwa na wahamiaji wakiwa safarini katika njia hizo kutoka mashariki na magharibi, yalifanywa na maafisa wa usalama, polisi, wanajeshi, maafisa wa uhamiaji na walinzi wa mipaka, ikilinganishwa na asilimia 29 ya manyanyaso yaliyofanywa na walanguzi.

Ripoti hiyo inaigawa Ikweta ya Afrika Kaskazini katika sehemu tatu na kueleza kila aina ya madhila. Wengine walizuiliwa ndani ya mabohari; baadhi walinyanyaswa kimwili kutoka kwa wasafirishaji wa watu kinyume na sheria na wengine walidhulumiwa kingono na kijinsia mikononi mwa maafisa wa serikali.

"Katika njia inayopitia Afrika Magharibi kuelekea Libya, maafisa wa usalama, maafisa wa uhamiaji na maafisa wa mipaka ndio haswa walihusishwa na dhuluma za kingono na kijinsia dhidi ya wahamiaji," Cochetel alisema wakati wa mahojiano katika makao makuu ya shirika la UNHCR.

Flüchtlinge aus Kongo
Wahamiaji kutoka Angola.Picha: Getty Images/AFP/J. Eisele

"Lakini tukiangazia manyanyaso mengine ya kimwili, mengi yamefanywa na walanguzi, wasafirishaji wa watu kinyume cha sheria pamoja na magenge mengine yanayohusishwa nao."

Hatua zaidi zahitajika kuimarisha ulinzi wa wahamiaji


Waandishi wa ripoti hiyo wamesema kazi zaidi yahitajika, kuimarisha ulinzi kwa wahamiaji, na kutoa njia bora mbadala za kisheria katika safari zao, huku wakitaja ufanisi mdogo kama kwa kuwakamata wahalifu wanaohusika na madhila hayo.

Vita, unyanyasaji chanzo cha ongezeko la wakimbizi duniani

"Ni sharti kuweko uwajibishwaji kamili wa makosa hayo ya jinai. Kunapaswa kuwe na upatikanaji wa mfumo wa kuwasilisha lawama na upatikanaji wa haki kwa waathiriwa wa usafirishaji kinyume cha sheria, punde wanapofika waendako salama," alisema Cochetel.

Aliongeza kuwa nchi ambako wahamiaji hutokea, hupitia na kuelekea zinapaswa kushirikishwa kwenye mfumo huo.


(AP)