Upinzani 'waongoza' uchaguzi Zambia
22 Septemba 2011Hatua hii ya Mahakama Kuu imekuja huku Tume ya Uchaguzi ikisema kuwa wezi wa mitandao wameunasa mtandao wao na kuweka matokeo ya uwongo yanayoonesha kuwa kiongozi wa upinzani Michael Satta anaongoza.
Amri hiyo ambayo ilitolewa kufuatia ombi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa serikali. Jaji wa Mahakama Kuu, Jane Kabuka, alisema wanavizuia vyombo vya habari kutangaza au kuchapisha matokeo yasiyo rasmi.
Katika toleo lake la jana (21.09.2011), gazeti binafsi la The Post lilikuwa na kichwa cha habari kuwa Satta ameshinda uchaguzi huo. Na hata baada ya pingamizi hilo la Mahakama Kuu, hivi leo tena gazeti hilo limeandika kuwa kiongozi huyo wa upinzani anaongoza kwa 59%.
Kwa upande mwengine, Tume ya Uchaguzi imesema wezi wa mitandao wameuingilia mtandao wake na kuchapisha matokeo ya uongo yanayoonesha kuwa kiongozi wa chama cha upinzani cha Patriotic Front, Michael Satta, anaongoza.
Msemaji wa Tume hiyo, Cris Akufuna, amesema kutokana na hitilafu hiyo maafisa wake wanafanyakazi kuhakiki zaidi ya mara mbili matokeo kutoka maeneo mbalimbali.
Amesema mchakato huo umesababisha kuchelewa kutolewa kwa matokeo, hali ambayo imeanza kuzua hofu ya kwamba matokeo ya uchaguzi huo yamefanyiwa hila.
Kwa mujibu wa matokeo ya hivi karibuni yaliyothibitishwa na Tume hiyo, kutoka majimbo 33 kati ya 150, kiongozi wa upinzani Michael Satta anaongoza akiwa na kura 265,843 dhidi ya Rais wa sasa, Rupiah Banda, kutoka chama tawala cha MMD aliyepata kura 192,936.
Katika maeneo kadhaa tayari washabiki wa kiongozi huyo wa upinzani wameanza kusherehekea wakiamiani kuwa kiongozi wao ameshinda.
Rais Banda anatarajiwa kupata kura nyingi katika maeneo ya mikoani, ambako kuna uwezekano wa utaratibu wa matokeo kutolewa kuwa wa taratibu, kuliko maeneo ambayo ni ngome ya upinzani, ambayo ni mjii mkuu Lusaka na maeneo ya Ukanda wa Shaba, ambako ndiko kitovu cha uchumi wa Zambia.
Hata hivyo, kwa mujibu wa duru za habari ni mapema mno kusema kuwa iwapo Michael Satta, maarufu kwa jina la King Cobra, yuko katika nafasi nzuri ya kushinda na kukiondoa katika urais chama tawala kwa mara ya kwanza tokea kumalizika kwa mfumo wa chama kimoja mwaka 1991.
Akufuna amesema bado wanaendelea kupokea matokeo kutoka maeneo mbalimbali na kwamba mpaka itakapofika leo jioni watatangaza matokeo rasmi.
Mwandishi: Aboubakary Liongo/Reuters/AFP
Mhariri: MohaMmed Abdul-Rahman